• Nairobi
  • Last Updated May 15th, 2024 8:55 PM
Hatukudhamini utafiti wa Infotrak kwa nia mbaya, Haki Africa yajitetea

Hatukudhamini utafiti wa Infotrak kwa nia mbaya, Haki Africa yajitetea

NA CHARLES WASONGA

SHIRIKA la kutetea haki za binadamu, Haki Africa, limejitetea dhidi ya madai kuwa lilidhamini kura ya maoni kuhusu umaarufu wa wanasiasa wa kaunti ya Mombasa kwa lengo ya kuwadunisha wanasiasa fulani na kuwatukuza wengine.

Kura hiyo iliendeshwa na kampuni ya utafiti ya Infotrak.

Mfanyabiashara wa Mombasa Suleiman Shabhal alisema utafiti huo ambao ulionyesha kuwa angeshindwa na Mbunge wa Mvita Abdulswamad Shariff Nassir, ulilenga kumdunisha.

“Ajenda ya Haki Africa sio nyingine ila kunishutumu na kunidunisha usiku na mchana. Sasa wametoa matokeo ya kura ya maamuzi ambayo haiakisi jinsi wakazi wa Mombasa watakavyopiga kura Agosti 9,” akasema kupitia ukurasa wake wa Facebook.

Lakini akiongea na wanahabari dakika chache baada ya kutolewa kwa matokeo ya kura hiyo Jumapili, Nairobi, Afisa wa Masuala ya Sheria Salwa Salim katika shirika hilo alisema lengo kuu la utafiti huo lilikuwa ni kutambua maeneo ambayo fujo zinaweza kutokea kuelekea uchaguzi mkuu.

“Wakati kama huu kuna masuala kadha ya kiusalama ambayo yamehusishwa na uchaguzi kama vile utovu wa usalama na ukosefu wa ajira. Kwa mfano leo (Jumapili, Machi 20, 2022) kuliripotiwa kisa ambapo genge la wahalifu liliwashambulia wakazi katika eneo la Kongowea, eneobunge la Nyali. Majeraha yalitokea na tunashuku kuwa mashambulio kama haya yanahusishwa na kampeni za uchaguzi,” akasema Bi Salim.

Awali, Afisa Mkuu Mtendaji wa Haki Afrika Bw Hussein Khalid alikariri kuwa data iliyokusanywa katika utafiti huo sio wa kisiasa pekee bali italisaidia kubaini chama cha kisiasa ambacho kina uwezekano mkubwa wa kusababisha fujo kabla, wakati na baada ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

“Tunaendelea na uchunguzi kubaini jinsi visa vya utovu wa usalama vinahusishwa na Uchaguzi Mkuu. Hii itatusaidia kutambua maeneo ambako kuna hatari ya kutokea ghasia za kisiasa ili kufuatilia. Aidha, data hiyo itatusadia kuweka mikakati ya mapema kuzuia kutokea kwa ghasia hizo,” akaeleza.

Kulingana na matokeo ya utafiti huo uliofanyika kati ya Machi 6, na 12, 2022 Bw Nassir angeibuka mshindi ikiwa uchaguzi mkuu ungefanyika wakati huo.

Mbunge huyo ambaye pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Bunge kuhusu Uwekezaji (PIC) ndiye angemrithi Joho kwa kupata uungwaji mkono kutoka kwa asilimia 48 ya waliohojiwa.

Ameshinda Bw Shabhal ambaye alipata asilimia 18 ya uungwaji huku nambari tatu akiwa ni Seneta wa zamani wa Mombasa Hassan Omar Sarai aliyepata uungwaji wa kima cha asilimia 5.

Mbunge wa Kisauni Ali Mbogo alipata asilimia 4 huku Naibu Gavana William Kingi akipata asilimia 1.

Jumla ya watu 2,400 walihojiwa katika utafiti huo katika maeneo bunge yote sita katika kaunti ya Mombasa.

Katika kiti cha useneta, seneta wa sasa Mohammed Faki aliyepata uungwaji mkono kutoka asilimia 21 ya wapiga kura akifuatwa na Hamisi Mwaguya aliyepata asilimia 5 huku Hashimu Mwidau akipata asilimia 2.

Mwakilishi wa Kike wa Mombasa Asha Hussein Mohammed angeshinda tena kiti hicho endapo uchaguzi mkuu ungefanya wakati ambapo utafiti huu uliendeshwa kwani aliibuka bora zaidi kwa uungwaji mkono wa asilimia 17.

Anafuatwa na Bi Zamzam Mohammed aliyepata asilimia 10 huku Bi Fatma Barayan Bakari akiungwa mkono na asilimia 5 ya wapiga kura wa Mombasa waliohojiwa na watafiti wa Infotrack.

  • Tags

You can share this post!

Liverpool wapewa Man-City, Palace wakivaana na Chelsea...

Leicester City wakomoa Brentford na kupaa hadi 10-bora...

T L