• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 7:12 PM
Liverpool wazamisha Chelsea na kutwaa Kombe la FA kwa mara ya kwanza tangu 2006

Liverpool wazamisha Chelsea na kutwaa Kombe la FA kwa mara ya kwanza tangu 2006

Na MASHIRIKA

LIVERPOOL walidumisha uhai wa matumaini ya kujizolea mataji manne msimu huu baada ya kupepeta Chelsea kwa penalti 6-5 na kunyanyua Kombe la FA kwa mara ya kwanza tangu 2006 mnamo Jumamosi ugani Wembley.

Mechi hiyo ilirejesha kumbukumbu za fainali ya Carabao Cup mwishoni mwa Februari ambapo Liverpool walishinda Chelsea kwa penalti 11-10 ugani Wembley baada ya gozi hilo pia kukamilika kwa sare tasa.

Mnamo Jumamosi, kipa Alisson Becker alipangua penalti ya Mason Mount na kuachia Kostas Tsimikas jukumu la kushindia Liverpool taji la pili msimu huu.

Chini ya kocha Jurgen Klopp, Liverpool bado wanafukuzia ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na watakutana na Real Madrid kwenye fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Mei 28, 2022 jijini Paris, Ufaransa.

Liverpool walianza mechi kwa matao ya juu huku Luis Diaz na Andrew Robertson wakishuhudia makombora yao yakibusu mwamba wa lango la Chelsea. Pigo pekee kwa Liverpool ni majeraha ambayo huenda yakawaweka nje wanasoka Mohamed Salah na Virgil van Dijk. Salah aliondolewa ugani katika kipindi cha kwanza huku beki na nahodha Van Dijk akiondolewa mwishoni mwa kipindi cha pili.

Matokeo dhidi ya Liverpool yalikuwa ya kusikitisha zaidi ikizingatiwa kwamba walikuwa na nafasi kadhaa za kufunga mabao kupitia kwa Marcos Alonso aliyeshuhudia mojawapo ya makombora yake likibusu mhimili wa lango la wapinzani wao na jingine likidhibitiwa vilivyo na Alisson. Chelsea kwa sasa ndicho kikosi cha kwanza kuwahi kupoteza fainali tatu mfululizo za Kombe la FA.

Sadio Mane alipoteza penalti yake kwa upande wa Liverpool baada ya kuzidiwa ujanja na kipa Edouard Mendy.

Kufikia sasa, Liverpool wanakamata nafasi ya pili kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 86, tatu nyuma ya vinara Manchester City. Liverpool watamenyana na Southampton katika EPL mnamo Mei 17, 2022 kabla ya kukamilisha ligi dhidi ya Wolverhampron Wanderers mnamo Mei 22, 2022.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Ruto aahidi kuwalainishia Wakenya maisha akichaguliwa rais

Washirika wa Mudavadi watetea MoU yake na Ruto

T L