• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Washirika wa Mudavadi watetea MoU yake na Ruto

Washirika wa Mudavadi watetea MoU yake na Ruto

NA SHABAN MAKOKHA

WASHIRIKA wa Musalia Mudavadi na Moses Wetang’ula wametetea mkataba kati ya vyama vya ANC, Ford Kenya na UDA cha Naibu Rais William Ruto kabla ya uchaguzi mkuu wa Agosti 9.

Seneta wa Kakamega Cleophas Malala, aliyekuwa seneta wa Kakamega Boni Khalwale, Mwakilishi wa kike wa kaunti ya Vihiga Beatrice Adagala na mbunge wa Mumias Mashariki Benjamin Washiali waliahidi kumzolea Dkt Ruto asilimia 70 ya kura za eneo la Magharibi mwa Kenya na kumwezesha kuunda serikali ijayo.

Viongozi hao walisema kwamba wanaweza kutimiza hilo na wakapuuza wakosoaji wao wanaolaumu Bw Mudavadi na Bw Wetang’ula wakisema hawawezi kushawishi asilimia 70 ya wapigakura wa eneo la Magharibi kumpigia kura Dkt Ruto.

Katika mkataba huo, asilimia 70 ya kura zote za Magharibi ni sharti la Bw Mudavadi na Bw Wetangula kupata asilimia 30 ya serikali itakayoundwa na muungano wa Kenya Kwanza Alliance ukishinda uchaguzi mkuu ujao.

Eneo la Magharibi la Kenya lina wapigakura 2.7 milioni waliosajiliwa kumaanisha viongozi wa ANC na Ford Kenya ni lazima wahakikishe kura 1,586,665 zinamwendea Dkt Ruto.

Kwa mujibu wa takwimu za Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kaunti ya Kakamega ina wapigakura 743,736 ikifuatwa na Bungoma iliyo na wapigakura 559,850, Vihiga (272,409) na Busia (351,048) huku Trans Nzoia ikiwa na wapigakura 339,662.

Wakizungumza wakiwa mjini Kakamega wakati Bw Malala alimzindua Dkt Beatrice Inyangala kuwa mgombea mwenza wake wa kiti cha ugavana, viongozi hao walisema wana uwezo wa kuhakikisha Dkt Ruto anazoa kura 1.5 milioni katika eneo la Magharibi.

Bw Malala alisema kwamba vyama hivyo viwili vilivyo na uungwaji mkono mkubwa eneo la Magharibi vitatimiza masharti yaliyo kwenye mkataba wao na Dkt Ruto.

“Kama wanajeshi wa Kenya Kwanza eneo hili, tumefanya kampeni kali ambazo zitatupa viti vingi katika eneo hili na kura nyingi kuwezesha eneo letu kupata asilimia 30 katika serikali ijayo,” akasema Bw Malala.

Bw Khalwale alishambuliwa na wanachama wa muungano wa Azimio chini ya kiongozi wa ODM Raila Odinga ambao walidai ni mlima kwa Bw Mudavadi na Wetang’ula kutimiza waliyokubaliana na Dkt Ruto.

“Wanafanyia mzaha wazo zuri kuhusu eneo la Magharibi. Watuambie eneo la Magharibi litanufaika vipi katika muungano wa Azimio. Nilicho na hakika nacho ni kuwa watu wa Magharibi ya Kenya watakuwa kwenye vyeo vya juu katika serikali ya Dkt Ruto tukitimiza makubaliano hayo na hata tukikosa kuyatimiza,” akasema Bw Khalwale.

Awali, mbunge wa Shinyalu Justus Kizito alikuwa ameshambulia Mudavadi na Wetang’ula akidai itakuwa vigumu kwao kutimiza makubaliano yao na Dkt Ruto.

  • Tags

You can share this post!

Liverpool wazamisha Chelsea na kutwaa Kombe la FA kwa mara...

Ngirici amteua mhasibu kuwa mgombea mwenza

T L