• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 1:13 PM
Macho kwa Cheptai kivumbi kikinukia kwenye mbio za nyika za kitaifa

Macho kwa Cheptai kivumbi kikinukia kwenye mbio za nyika za kitaifa

Na AYUMBA AYODI

ALITANGAZA kuwasili kwake kwenye mashindano ya humu nchini na kimataifa kwa kishindo mwaka 2017.

Mtimkaji Irene Cheptai,29, alibeba taji lake la kwanza la Mbio za Nyika kabla ya kuongeza umalkia wa dunia jijini Kampala, Uganda baada ya kusikitisha katika nafasi ya 13 mjini Bydgoszcz, Poland mwaka 2013 na Guiyang, Uchina mwaka 2015.

Kisha, Cheptai alichukua likizo ya uzazi kabla ya kurejea 2019 akishiriki mbio za barabarani na zile za uwanjani bila mafanikio makubwa, huku jeraha la kinena likifanya maisha yake kuwa magumu.

Kwa mfano, mama huyo wa mtoto mmoja alikamilisha mbio za New Delhi Half Marathon nchini India katika nafasi ya nne mnamo Oktoba 2019 na kukamata nafasi hiyo tena katika mbio hizo Novemba 2020, katika msimu ambao ulivurugwa na mkurupuko wa virusi vya corona.

Hata hivyo, Cheptai, ambaye alishikilia nafasi ya pili katika mbio za nyika za eneo la North Rift wikendi iliyopita nyuma ya Vicotty Chepng’eno, ana ari ya kupata makali aliyokuwanayo 2017, mwaka huu.

Cheptai ni miongoni mwa wanariadha watakaotifua vumbi katika mbio za nyika za kitaifa zinazodhaminiwa na kampuni ya kamari ya Lotto zitakazofanyika uwanjani Ngong Racecourse.

Mashindano hayo yalipigwa jeki hapo Februari 11 wakati wakfu wa Lotto ulizindua ufadhili wa Sh7 milioni kwa makala haya.

Huu ni mwaka wa sita Lotto imedhamini mashindano hayo yakatakayotumiwa kuchagua timu ya taifa itakayoshindania ubingwa wa Bara Afrika mnamo Machi 6 jijini Lome, Togo. Mbio hizo za Afrika ziliahirishwa kutoka 2020 hadi 2021 kutokana na mkurupuko wa virusi vya corona.

Cheptai, ambaye anafanya mazoezi yake mjini Iten chini ya kocha Barnaba Chirchir, atatoana jasho na wakimbiaji wengine watatu ambao wametwaa taji la kinadada mara moja katika kitengo cha watu wazima. Watimkaji hao ni bingwa mtetezi Sheila Chelangat kutoka timu ya polisi, mshindi wa 2016 Alice Aprot (magereza) na 2018 Stacy Ndiwa (polisi).

“Malengo yangu sio kuibuka mshindi, bali kupima mwili wangu ninapoendelea kupona jeraha linalonisumbua la kinena,” alisema Cheptai ambaye lengo lake kubwa ni kupata tiketi ya kupeperusha bendera ya Kenya katika mbio za mita 10,000 kwenye michezo ya Olimpiki jijini Tokyo, Japan baadaye mwaka huu.

Akifanikiwa, itakuwa mara ya kwanza Cheptai kuwa katika Olimpiki, ingawa aliwahi kutimka katika Riadha za Dunia 2015 jijini Beijing na 2017 jijini London alipokamilisha katika nafasi ya saba mara yote mbili katika mbio hizo za mizunguko 25.

Hellen Obiri (Majeshi-KDF), ambaye alinyakua taji la mbio za kitaifa za nyika mwaka 2020 kabla ya kuongeza lile la dunia mwaka uo huo, ameamua kushiriki kitengo cha mbio mseto za kupokezana vijiti.

Wengine ni pamoja na bingwa wa Idara ya Magereza Rosemary Wanjiru na mshindi wa medali ya dhahabu ya chipukizi wasiozidi umri wa miaka 20 kwenye Mbio za Nyika za Dunia 2019, Beatrice Chebet ambaye atawakilisha timu yake ya South Rift.

Afisa Mkuu Mtendaji wa Lotto,  Joan Mwaura, alipokeza mwenzake kutoka Shirikisho la Riadha Kenya (AK), Susan Kamau, hundi hiyo. Kamau aliandamana na naibu wa mwekahazina wa AK Dimmi Kisalu na wanakamati Barnaba Korir na Benjamin Njoga katika afisi za shirikisho hilo jijini Nairobi.

Korir alialika mashabiki kufika Ngong Racecourse kwa wingi kushangilia timu zao akiongeza kuwa mashindano hayo yataandaliwa kwa kuzingatia masharti ya afya ya kuzuia uenezaji wa virusi vya corona.

“Tutakuwa na waelekezi katika sehemu muhimu wakiwa pia na vyeuzi. Kutakuwepo pia sehemu za kunawa mikono,” alisema Korir na kufichua kuwa timu 19 zitawania ubingwa katika mashindano hayo yatakayoanza saa tatu asubuhi.

Mbali na maeneo 12 na timu nne za taasisi, AK imealika Shirika la Kenya la Wanyamapori (KWS), shirika la huduma ya vijana kwa kitaifa (NYS) na timu za wakimbizi.

“Tuna furaha kuwa karibu wakimbiaji wote tunaoona wanaweza kutuwakilisha Olimpiki katika mbio za mita 10,000 na mita 5,000 watashiriki,” alisema na kuongeza kuwa kufutiliwa mbali kwa mbio za kilomita 21 za Ras Al Khaimah nchini Milki za Kiarabu zilizofaa kufanyika Februari 19, ni baraka.

“Sasa tuko hapa na wakimbiaji wengi ambao walilenga kususia mashindano ya kitaifa na tutarajie kivumbi Jumamosi,” alieleza Korir.

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE

  • Tags

You can share this post!

COVID-19: Kocha Jurgen Klopp akosa kusafiri Ujerumani...

DROO YA KOMBE LA FA: Leicester City wapewa Man-United huku...