• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 2:59 PM
DROO YA KOMBE LA FA: Leicester City wapewa Man-United huku Man-City wakikutanishwa na Everton

DROO YA KOMBE LA FA: Leicester City wapewa Man-United huku Man-City wakikutanishwa na Everton

Na MASHIRIKA

EVERTON watakuwa wenyeji wa viongozi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) Manchester City kwenye robo-fainali za Kombe la FA msimu huu huku Manchester United wakikutanishwa na Leicester City uwanjani King Power.

Chini ya kocha Carlo Ancelotti, Everton walipepeta 5-4 kwenye raundi ya tano na kufuzu kwa hatua hiyo ya nane-bora itakayonogeshwa katika wikendi ya Machi 20-21.

Mchuano utakaochezewa ugani King Power utakutanisha vikosi viwili vinavyowania nafasi ya kutia kapuni ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu. Kufikia sasa, Leicester wanashikilia nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 43, mbili pekee nyuma ya Man-United ambao ni wa pili.

Man-City ya kocha Pep Guardiola inadhibiti kilele cha jedwali la EPL kwa alama 50 huku pengo la pointi 13 likitamalaki kati yao na nambari saba Everton.

Katika mechi nyinginezo za robo-fainali, Bournemouth ya Ligi ya Daraja la Kwanza nchini Uingereza (Championship) itakutana na Southampton ugani Vitality huku wanafainali wa msimu wa 2019-20 Chelsea wakiwaalika Sheffield United uwanjani Stamford Bridge.

Southampton walijikatia tiketi ya robo-fainali baada ua kuwapokeza Wolves kichapo cha 2-0 ugani Molineux huku Chelsea wakidengua Barnsley kwa ushindi mwembamba wa 1-0 ugenini.

Man-City wanaofukuzia mataji manne katika kampeni za msimu huu walifuzu kwa hatua ya nane-bora kwenye Kombe la FA baada ya kutandika Swansea City 3-1 ugani Liberty huku Man-United wakikomoa West Ham United ya kocha David Moyes 1-0 uwanjani Old Trafford kwenye raundi ya tano.

DROO YA ROBO-FAINALI ZA KOMBE LA FA:

Everton na Manchester City

Bournemouth na Southampton

Leicester City na Manchester United

Chelsea na Sheffield United

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Macho kwa Cheptai kivumbi kikinukia kwenye mbio za nyika za...

Matatu iliyoua abiria 9 ilikiuka kanuni za kudhibiti...