• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 6:50 AM
Macho kwa Kipyegon na Jepchirchir mbio za barabarani Latvia 

Macho kwa Kipyegon na Jepchirchir mbio za barabarani Latvia 

NA GEOFFREY ANENE

MBIVU na mbichi kuhusu nani mkali kwenye Riadha za Dunia za Barabarani itajulikana miamba Kenya na Ethiopia watakapofufua uhasama mnamo Jumapili jijini Riga nchini Latvia.

Wanariadha kutoka mataifa hayo mawili wanapigiwa upatu kufanya vyema katika makala hayo ya kwanza, ingawa Wakenya pia watapata ushindani mkali kutoka Afrika Kusini, Uganda, Amerika, Canada, Norway na Bahrain.

Jumla ya wanariadha 347 kutoka mataifa 57 watashiriki.

Mabingwa wa Olimpiki Faith Kipyegon (mbio za mita 1,500) na Peres Jepchirchir (marathon) wanaongoza orodha ya Wakenya wanaopigiwa upatu kutwaa mataji ya maili moja na nusu-marathon, mtawalia.

Bingwa wa dunia Kipyegon amekuwa na msimu mzuri mwaka huu ambapo aliweka rekodi za dunia mbio za 1,500, maili moja na kilomita tano.

Atajiweka pazuri kuibuka mwanariadha bora duniani wa mwaka 2023 wa akina dada akishinda maili moja Jumapili.

Jepchirchir atavizia taji lake la tatu la dunia la kilomita 21 baada ya kutawala mwaka 2016 na 2020.

Akifanikiwa, bingwa wa New York City Marathon mwaka 2021 na Boston mwaka 2022 Jepchirchir atakuwa mwanadada wa nne kushinda nusu-marathon duniani mara tatu baada ya Tegla Loroupe (Kenya), Paula Radcliffe (Uingereza) na  Lornah Kiplagat (Uholanzi).

Bingwa wa Barcelona Half Marathon Irine  Kimais pamoja na Margaret Kipkemboi na Catherine Relin wanakamilisha orodha ya Wakenya watakaoshiriki nusu-marathon Oktoba.

Katika nusu-marathon ya wanaume, Kenya pia inawakilishwa na mshindi wa Ras Al-Khaimah Half Marathon Benard Kibet pamoja na Charles Langat, Sabastian Sawe na Daniel Simiu.

Ushindani mkali utatoka kwa Waethiopia akiwemo Jemal Yimer, Mganda Andrew Rotich Kwemoi, Stephen Mokoka kutoka Afrika Kusini, Ibrahim Hassan (Djibouti), Mohamed Reda (Morocco) Tomoki Ota (Japan).

Kambini Kenya, macho pia yatakuwa kwa Reynold Cheruiyot (maili moja) na Beatrice Chebet (kilomita tano).

  • Tags

You can share this post!

Biblia ya lugha ya Kipokomo yazinduliwa

Mwanamitindo Milka Mukami kuwakilisha Kenya kwa shindano la...

T L