• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Malkia Strikers tayari kuelekea Brazil baada ya Mozzartbet kuiokoa

Malkia Strikers tayari kuelekea Brazil baada ya Mozzartbet kuiokoa

Na JOHN KIMWERE

AKINA dada wa timu ya taifa ya mchezo wa voliboli maarufu Malkia Strikers wapo tayari kuelekea nchini Brazil kwa mazoezi ya miezi miwili kujinolea fainali za Kombe la Dunia (FIVB) zitakaofanyika Septemba 23 hadi Oktoba 25 nchini Uholanzi na Poland.

Vipusa hao watakaoungana na Cameroon kuwakilisha Afrika kwenye ngarambe hiyo wamejaa furaha tele baada ya shirika la kubeti la Mozzartbet kufadhili tikiti za ziara hiyo.

Kando na ufadhili wa tiketi pia walipata ufadhili wa kitita cha Sh10 milioni.

Naibu nahodha wa kikosi hicho Noel Murambi anasema, ”Tunashukuru Mozzarbet kwa kusikia kilio chetu ambapo tunaahidi kuwa tutajitahidi tuwezavyo kuhakikisha tunapata matunda mazuri hasa kufuzu kushiriki mechi za raundi ya pili.”

Naye mwenyekiti wa Shirikisho la Voliboli ya Kenya (KVF) Kioni Waithaka anatoa wito kwa wachezaji walioteuliwa kwenye kikosi hicho kujituma kisawasawa na kuonyesha mchezo mzuri ili kudhihirisha kuwa walipata nafasi hiyo kihalali.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Voliboli ya Kenya (KVF), Kioni Waithaka (kushoto) apokea hundi ya Sh10 milioni kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mozzartbet, Kenya, Sasa Krneta. PICHA | JOHN KIMWERE

Kadhalika Kioni alishukuru washika dau wote waliowaunga mkono katika uongozi wa shirikisho katika kipindi chake na kuwaomba waendelea kuwa na moyo huo pia wawe makini kuchagua viongozi wenye nia ya kupaisha mchezo huo.

Kulingana na katiba ya KVF, Kioni hatakuwa anagombea wadhifa wowote kwenye uchanguzi ujao.

Baada ya mazoezi Brazil warembo hao chini ya kocha mkuu, Paul Bitok na naibu wake, Japheth Munala watasafiri nchini Serbia kwa mazoezi ya siku kumi pia kushiriki mechi mbili za kupimana nguvu dhidi ya wenyeji Serbia na Colombia.

Kocha Paul Bitok anasema: ”Baada ya kutathimini wapinzani wetu kwenye kundi A, hatuna lingine mbali lazima tupambane mwanzo mwisho kuhakikisha tunajikatia tiketi ya mechi za raundi ya pili.”

Kikosi kinatarajia kusafiriki nchini Brazil kinajumuisha: Mercy Moim, Noel Murambi, Veronica Adhiambo, Meldinah Sande, Yvonne Wavinya, Edith Wisa, Belinda Barasa, Madgalene Mwende, Lorine Chebet, Gladys Ekaru, Sharon Chepchumba, Violet Makuto, Veronica Kilabat, Emmaculate Nekesa, Agrippina Kundu na Veronica Makokha.

Waliotemwa ni Trizah Atukah, Faith Imondia, Emmaculate Chemtai na Pamela Jepkirui.

  • Tags

You can share this post!

Spurs wasajili kiungo Bissouma kutoka Brighton

NMG yasema waziwazi haiegemei mrengo wowote wa kisiasa

T L