• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 9:35 PM
Malkia Strikers warejea uwanjani kesho dhidi ya Serbia

Malkia Strikers warejea uwanjani kesho dhidi ya Serbia

ELIAS MAKORI na JOHN ASHIHUNDU

BAADA ya kupoteza mechi mbili mfululizo dhidi ya Japan na Korea Kusini mtawaliwa, timu ya taifa ya voliboli maarufu kama Malkia Strikers itarejea uwanjani Alhamisi alfajiri kuvaana na Serbia.

Katika mechi yao ya nne kwenye Kundi B, kikosi hicho chini ya kocha Paul Bitok kitapepetana na Jamhuri ya Dominic Jumamosi, kabla ya kumaliza mechi za kundi hilo Jumatatu itakapokabiliana na Brazil.

Malkia Strikers ilicheza kwa ujasiri mkubwa Jumanne, kabla ya kushindwa na Korea Kusini kwa seti 3-0 za 25-14, 25-22 na 26-24.

Katika mechi za awali, timu hiyo ilibwagwa na Japan 3-0 (25-15, 25-11 na 25-23) Jumapili kabla ya kuchapwa na Korea Kusini.

Kikosi hicho kilikuwa kikifanya marejeo kwenye michezo hiyo baada ya miaka 16, lakini kikashangaza kwa kucheza kwa kiwango cha juu na hata kuongoza kwa 6-1, kabla ya kulegea baadaye katika mechi hiyo iliyochezewa ukumbi wa Ariake Arena.

Malkia Strikers walicheza vizuri zaidi kiasi cha kukaribia kushinda seti ya mwisho ambayo waliipoteza kwa 24-25.

Wapinzani walikuwa wameshinda seti mbili za kwanza kwa 25-14 na 25-22 kabla ya kuponea chupuchupu kwenye seti ya mwishoambayo ilimalizika kwa 26-24.

Nyota wa KCB, Sharon Chepchumba aliibuka mfungaji wa mabao mengi kwa upande wa Malkia baada ya kufikisha 14, huku mfungaji bora wa Korea Kusini Kim Heejin akifunga 20.

“Ningependa kuwapongeza wachezaji kwa kuzua upinzani mkali. Tulianza vizuri, kabla ya wachezaji kuchanganyikiwa na kupoteza muelekeo,” alisema Bitok.

“Tulikuwa na nafasi nzuri ya kushinda seti ya tatu, lakini hatukuelewana vyema uwanjani. Timu haikucheza jinsi tulivyopanga,” aliongeza.

Kenya ilishiriki kwa mara ya kwanza katika michezo ya Olimpiki mnamo 2000 na 2004, na ni miongoni mwa timu zilizowekewa matumaini ya kufanya vyema.

You can share this post!

TENISI: Naomi Osaka aondolewa mapema kwenye Olimpiki 2020

Mwili wa mwanamke wapatikana umetupwa kisimani