• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 7:55 AM
Malkia wa ulimwengu wa soka kujulikana Uingereza ikipambana na Uhispania

Malkia wa ulimwengu wa soka kujulikana Uingereza ikipambana na Uhispania

Na MASHIRIKA

BAADA ya mwezi mzima wa patashika na fataki nchini New Zealand na Australia, malkia wapya wa Kombe la Dunia hatimaye watajulikana leo Jumapili, Agosti 20, 2023, Uhispania watakapovaana na Uingereza jijini Sydney, Australia.

Mshindi wa kipute hicho atatia kibindoni kima cha Sh619 milioni huku nambari mbili akiridhika na Sh435 milioni.

Uhispania wanawania taji lao la kwanza katika mashindano ya haiba kubwa. Sawa na Uingereza, pia ni mara yao ya kwanza katika historia kutinga fainali ya Kombe la Dunia.

Katika makala yao ya kwanza ya dimba hili, Uhispania waliambulia nafasi ya 12 mnamo 2019 nchini Ufaransa.  Walianza kampeni za mwaka huu kwa ushindi wa 3-0 dhidi ya Costa Rica katika Kundi C kabla ya kuponda Zambia 5-0 na kukubali kichapo cha 4-0 kutoka kwa Japan.

Walikung’uta Uswisi 5-1 katika hatua ya 16-bora kabla ya kupepeta Uholanzi 2-1 kwenye robo-fainali kisha kutandika miamba Uswidi 2-1 katika nusu-fainali.

Ushindi dhidi ya Uswisi ulikuwa wa kwanza kwa Uhispania kusajili kwenye hatua za muondoano za kipute cha haiba kubwa katika ulingo wa soka.

Kufikia sasa, Uhispania ndio wanaojivunia kupachika wavuni mabao mengi zaidi (17) kwenye fainali za Kombe la Dunia mwaka huu na watajibwaga ugani wakipigiwa upatu wa kutatiza Uingereza.

Chini ya kocha Sarina Wiegman, huu ni mwaka wa pili mfululizo kwa warembo wa Uingereza kunogesha fainali ya mashindano ya haiba kubwa. Walitawazwa mabingwa wa Euro 2022 baada ya kupeteta Ujerumani 2-1 mbele ya mashabiki 87, 192 ugani Wembley.

Uingereza walifungua kampeni zao za Kundi D kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Haiti kabla ya kupokeza Denmark kichapo sawa na hicho. Walicharaza China 6-1 katika pambano la mwisho kundini kabla ya kufunga Nigeria penalti 4-2 kufuatia sare ya tasa katika hatua ya 16-bora. Walipepeta Colombia 2-1 katika robo-fainali kisha wakadengua wenyeji Australia kwa 3-1 katika hatua ya nne-bora.

Fainali ya Agosti 20, 2023 itakuwa ya nne mfululizo katika mapambano ya haiba kubwa kwa kocha Wiegman kushiriki. Hata hivyo, atapania kuepuka masaibu ya 2019 ambapo kilichokuwa kikosi chake cha Uholanzi kilikubali kichapo cha 2-0 kutoka kwa Amerika kwenye fainali ya Kombe la Dunia.

Warembo wake watajitosa ulingoni wakilenga kuendeleza makali ya 2022 yaliyowavunia ushindi wa 2-1 dhidi ya Uhispania katika robo-fainali za Euro.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

HABARI YA KIPEKEE: Mwanamume aliyejiteketeza kwa mafuta ya...

Mwanamume Murang’a ajitoa uhai kwa kukosa Sh30, 000...

T L