• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 7:15 PM
Man-City kumsajili Joao Felix wa Atletico ili kuziba pengo la Aguero anayehemewa na Barcelona

Man-City kumsajili Joao Felix wa Atletico ili kuziba pengo la Aguero anayehemewa na Barcelona

Na MASHIRIKA

MANCHESTER wamefichua mpango wa kumsajili fowadi chipukizi wa Atletico Madrid, Joao Felix, ili awe kizibo cha mshambuliaji matata raia wa Argentina, Sergio Aguero anayehusishwa pakubwa na Barcelona.

Licha ya kukosa maarifa ya Aguero ambaye ni mfungaji bora wa muda wote kambini mwao, Man-City wamejivunia kampeni za kuridhisha msimu huu na matokeo bora ambayo wamesajili yanazidi kuweka hai matumaini yao ya kujitwalia jumla ya mataji manne muhula huu.

Zaidi ya kufukuzia ufalme wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Man-City wangali katika mbio za kuwania taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA), Kombe la FA na League Cup.

Kati ya wanasoka ambao Man-City wamekuwa wakitegemea kuongoza safu yao ya uvamizi baada ya Aguero kuwa mwepesi wa kupata majeraha kuanzia mwisho wa msimu uliopita wa 2019-20, ni Raheem Sterling, Kevin De Bruyne, Ferran Torres na Gabriel Jesus.

Japo Man-City wana azma ya kumdumisha Aguero uwanjani Etihad kwa mwaka mmoja zaidi ila kwa mshahara uliopunguzwa, sogora huyo ambaye mkataba wake unakamilika mwishoni mwa msimu huu, ana malengo ya kuhamia Barcelona nchini Uhispania.

Tangazo la kuondoka kwake linatarajiwa wakati wowote mwezi ujao, na Man-City wanatarajiwa kumtwaa Joao ili kujaza pengo lake. Mwanasoka mwingine ambaye anahusishwa pakubwa na Man-City ni chipukizi matata raia wa Norway ambaye kwa sasa anachezea Borussia Dortmund ya Ujerumani, Erling Haaland.

Rais mpya wa Barcelona, Joan Laporta, amesisitiza kwamba ana azma ya kumdumisha Lionel Messi uwanjani Camp Nou ili ashirikiane na Aguero pamoja na wanasoka wengine wawili wanaohemewa na Barcelona kutoka Inter Milan. Mafowadi hao wanaohusishwa na Barcelona kutoka Italia ni Lautaro Martinez na mwenzake Romelu Lukaku ambaye pia amewahi kuchezea Everton na Manchester United.

Man-City waliwahi kujaribu kumsajili Joao mnamo 2019 kabla ya sogora huyo raia wa Ureno kubanduka Benfica na kutua uwanjani Wanda Metropolitano kusakatia Atletico waliojinasia huduma zake kwa Sh14 bilioni.

Kufikia sasa, Joao, 21, amefungia Atletico jumla ya mabao 19 kutokana na michuano 67. Kusajiliwa kwake kulichochewa na ulazima wa kikosi cha Atletico kinachonolewa na kocha Diego Simeone, kujaza pengo la fowadi Antoine Griezmann aliyeyoyomea Barcelona.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Ndani ya miaka 50 ya huduma ya uchungaji kwa Askofu Peter...

WHO yapuuzilia mbali ‘madhara’ ya chanjo ya...