• Nairobi
  • Last Updated May 13th, 2024 3:09 PM
Man-City wapepeta Real Madrid katika mkondo wa kwanza wa nusu-fainali ya UEFA ugani Etihad

Man-City wapepeta Real Madrid katika mkondo wa kwanza wa nusu-fainali ya UEFA ugani Etihad

Na MASHIRIKA

MANCHESTER City walitia guu moja ndani ya fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu baada ya kupokeza Real Madrid kichapo cha 4-3 katika mkondo wa kwanza wa nusu-fainali mnamo Jumanne usiku ugani Etihad.

Chini ya kocha Pep Guardiola, Man-City walianza mechi kwa matao ya juu na wakaweka kifua mbele na Kevin de Bruyne katika dakika ya pili baada ya kushirikiana vilivyo na Riyad Mahrez.

Gabriel Jesus alifunga bao la pili la Man-City katika dakika ya 11 kabla ya Karim Benzema kurejesha Real mchezoni mwishoni mwa kipindi cha pili. Phil Foden alikamilisha krosi ya Fernandinho Luiz Roza katika dakika ya 53 na kuwapa Man-City uongozi wa 3-1.

Ingawa hivyo, Vinicius Junior alimpiku Fernandinho na kujaza kimiani bao la pili la Real waliofungiwa penalti na Benzema kunako dakika ya 82. Goli jingine la Man-City lilifumwa wavuni na Bernardo Silva katika dakika ya 74.

Man-City sasa watavaana na Real katika marudiano ya nusu-fainali za UEFA jijini Madrid, Uhispania mnamo Mei 4, 2022. Mshindi baada ya mikondo miwili atakutana na Liverpool au Villarreal kwenye fainali itakayosakatiwa ugani Stade de France jijini Paris mnamo Mei 28, 2022.

Man-City walitinga nusu-fainali za UEFA muhula huu baada ya kudengua Atletico Madrid kwenye hatua ya nane-bora kwa bao 1-0. Kwa upande wao, Real walilipiza kisasi dhidi ya Chelsea waliowabandua kwenye nusu-fainali za UEFA msimu jana kwa mabao 3-1 na kuwang’oa kwa jumla ya magoli 5-4 kwenye robo-fainali.

Kufikia sasa, Man-City wanafukuzia mataji mawili msimu huu na wanaselelea kileleni mwa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa alama 80, moja pekee nyuma ya Liverpool wanaowania jumla ya mataji manne muhula huu.

Man-City hawajawahi kushindwa kwenye UEFA uwanjani Etihad tangu Septemba 2018 walipopokezwa kichapo cha 2-1 kutoka kwa Olympique Lyon ya Ufaransa. Kikosi hicho sasa kimepachika wavuni mabao 17 kutokana na mechi sita zilizopita za UEFA msimu huu huku wakibandua Sporting Lisbon ya Ureno na Atletico bila kufungwa goli kwenye hatua za 16-bora na robo-fainali mtawalia.

Iwapo Man-City wataingia fainali ya UEFA muhula huu, basi mkufunzi wao Pep Guardiola atakuwa kocha wa kwanza kung’oa Real kwenye kipute cha UEFA mara tatu. Ufanisi huo utamchochea zaidi Mhispania huyo aliyewahi kudhibiti mikoba ya Barcelona na Bayern Munich kuzolea waajiri wake taji la UEFA kwa mara ya kwanza katika historia.

Matumaini ya Real kutinga fainali za UEFA msimu huu yanabebwa na sogora Karim Benzema ambaye sasa amewafungia mabao tisa dhidi ya PSG, Chelsea na Man-City katika michuano mitano ya hatua ya 16-bora, robo-fainali na mkondo wa kwanza wa hatua ya nne-bora.

Benzema, 34, anajivunia mabao 14 katika UEFA kufikia sasa msimu huu na anaongoza orodha ya wafungaji bora wa Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) kwa magoli 25 baada ya kunogesha mechi 28.

Sawa na Man-City waliobebwa na Gabriel Jesus dhidi ya Watford kwa ushindi wa 5-1 ligini, Real walijitosa ugani wakiwa na motisha ya kupepeta Osasuna 3-1 katika mechi iliyopita ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) iliyoshuhudia Benzema akipoteza mikwaju miwili ya penalti.

Real wanaofukuzia taji la UEFA kwa mara 13, walikuwa wameshinda mechi sita mfululizo za awali ugenini katika mashindano yote huku wakifunga mabao matatu katika kila mojawapo ya mechi tatu za karibuni zaidi kabla ya kuendea Man-City.

Hakuna kikosi chochote kimewahi kushinda vikosi viwili tofauti vya EPL kwenye hatua za muondoano za UEFA ugenini katika msimu mmoja. Mechi ya Jumanne usiku ilikuwa ya saba kuwahi kukutanisha Real na Man-City katika UEFA. Real walishinda 1-0 katika michuano ya mikondo miwili ya nusu-fainali za 2015-16 kabla ya Man-City kulipiza kisasi kwa kushinda 2-1 katika mechi mbili za hatua ya 16-bora mnamo 2019-20.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Jinsi kampuni inavyoepushia wafugaji eneo kame kukadiria...

Mlinzi wa Ingwe kukaa nje miezi minne

T L