• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 3:16 PM
Man-City watandika Liverpool 4-1 katika EPL

Man-City watandika Liverpool 4-1 katika EPL

NA MASHIRIKA

MANCHESTER City waliweka hai matumaini ya kuhifadhi taji la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu kwa kukomoa Liverpool 4-1 ugani Etihad licha ya kukosa huduma za mvamizi matata Erling Haaland anayeuguza jeraha la kinena.

Liverpool walitangulia kuona lango la wenyeji wao kupitia kwa Mohamed Salah katika dakika ya 17 kabla ya Julian Alvarez, Kevin de Bruyne, Ilkay Gundogan na Jack Grealish kufungia Man-City.

Matokeo hayo yalidumisha Man-City katika nafasi ya pili jedwalini kwa alama 64 huku pengo la pointi 22 likiwatenganisha na Liverpool ambao wana mchuano mmoja zaidi wa akiba.

Man-City sasa wameshinda kila mojawapo ya mechi saba zilizopita katika mashindano yote, zikiwemo sita za mwisho ambazo zimewashuhudia wakiondoka ugani wakifungwa bao moja pekee.

Hadi walipodhalilisha Liverpool jana, Man-City walikuwa wameponda RB Leipzig ya Ujerumani 7-0 katika mkondo wa pili wa hatua ya 16-bora ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kabla ya kucharaza Burnley 6-0 katika robo-fainali ya Kombe la FA.

Miamba hao wanaonolewa na kocha Pep Guardiola walikuwa wamepoteza mechi mbili kati ya tatu dhidi ya Liverpool msimu huu, japo ushindi wa 3-2 waliouvuna katika raundi ya nne ya Carabao Cup mnamo Disemba 2022 ugani Etihad ulikomesha rekodi duni ya kutoangusha Reds mara tano mfululizo.

Aidha, walikuwa wamepoteza mechi moja pekee kati ya 13 za awali dhidi ya Liverpool katika EPL uwanjani Etihad, hiyo ikiwa mnamo Novemba 2015 ambapo walipepetwa 4-1.

Kwa kukomoa Liverpool, Man-City sasa wameshinda mechi nne mfululizo ligini msimu huu kwa mara ya kwanza.

Kichapo kutoka kwa Man-City kilikuwa cha tisa kwa Liverpool kupokea ligini na wamejizolea alama 12 pekee kutokana na mechi 14 za ugenini katika EPL muhula huu baada ya kupoteza mara nane na kufunga bao moja pekee katika michuano saba.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Wakazi 160,000 Tana River waumizwa na njaa

Mwisho wa maandamano ni Jumatatu – Gachagua

T L