• Nairobi
  • Last Updated May 6th, 2024 10:55 AM
Man-City wazamisha Atletico katika mkondo wa kwanza wa robo-fainali ya UEFA ugani Etihad

Man-City wazamisha Atletico katika mkondo wa kwanza wa robo-fainali ya UEFA ugani Etihad

Na MASHIRIKA

BAO la kipindi cha pili kutoka kwa Kevin de Bruyne liliwapa Manchester City ushindi wa 1-0 dhidi ya Atletico Madrid ya Uhispania katika mchuano wa mkondo wa kwanza wa robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Jumanne usiku ugani Etihad.

Atletico wanaonolewa na kocha Diego Simeone waliibana sana safu yao kwa kipindi kirefu hadi De Bruyne alipovurumisha kombora lililomwacha hoi kipa Jan Oblak katika dakika ya 70.

Bao hilo la De Bruyne lilichangiwa na kiungo mvamizi Phil Foden aliyeletwa uwanjani katika dakika ya pili. Kuja kwake kulibadilisha kasi ya mchezo na akamtatiza pakubwa beki Reinildo Mandava.

Kocha Pep Guardiola alisherehekea bao hilo la Man-City kwa mbwembwe kuonyesha jinsi alivyokuwa akilisubiri kwa hamu. Sasa anatarajiwa kuongoza kikosi chake kwa mchuano wa mkondo wa pili katika uwanja wa Wanda Metropolitano jijini Madrid mnamo Aprili 13, 2022.

Atletico walishuka dimbani wakipigiwa upatu wa kupepeta Man-City ikizingatiwa kwamba walidengua Manchester United kwenye hatua ya 16-bora msimu huu. Aidha, walibandua Liverpool waliokuwa mabingwa watetezi wa UEFA kwenye hatua ya 16-bora mnamo 2020-21 baada ya kuwachapa katika michuano yote ya mikondo miwili.

Chini ya Guardiola, Man-City walifuzu kwa robo-fainali za UEFA msimu huu baada ya kung’oa Sporting Lisbon ya Ureno kwa mabao 5-0 katika hatua ya 16-bora huku Atletico wakizamisha mashetani wekundu wa Man-United kwa jumla ya mabao 2-1.

Gozi dhidi ya Atletico mnamo Jumanne usiku ni mwanzo wa kibarua kigumu kwa Man-City wanaofukuzia mataji matatu muhula huu. Baada ya kuwa wenyeji wa Liverpool katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Aprili 10, 2022, miamba hao watarudiana na Atletico katika UEFA mnamo Aprili 13 nchini Uhispania kabla ya kukutana tena na Liverpool kwenye nusu-fainali ya Kombe la FA siku tatu baadaye ugani Wembley.

Kufikia sasa, Man-City wanaselelea kileleni mwa jedwali la EPL kwa alama 73, moja mbele ya nambari mbili Liverpool ambao pia wametandaza mechi 30. Mshindi wa pambano la Aprili 10, 2022 kati ya vikosi hivyo ugani Etihad huenda akatawazwa mfalme wa EPL msimu huu iwapo atasalia imara katika mechi saba zitakazosalia kwenye kampeni za kivumbi hicho.

Licha ya presha kali ya kuhifadhi taji la EPL, Man-City wana kiu ya kujizolea ufalme wa UEFA kwa mara ya kwanza katika historia. Tottenham Hotspur waliwang’oa kwenye robo-fainali za kipute hicho miaka mitatu iliyopita kabla ya Chelsea kuwakung’uta 1-0 kwenye fainali ya 2020-21 jijini Porto, Ureno.

Mbali na rekodi ya kutopigwa kwenye mechi saba zilizopita katika mashindano yote, Man-City walikuwa wameshinda mechi tisa mfululizo za UEFA ugani Etihad kabla ya Sporting kuwalazimishia sare tasa kwenye mkondo wa pili wa hatua ya 16-bora mnamo Machi 9.

Atletico kwa upande wao walijitosa ugani wakiwa na ari ya kuendeleza ubabe uliowawezesha kukomoa Alaves 4-1 katika Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) mnamo Aprli 2, 2022. Ushindi huo ulikuwa wa sita mfululizo kwa mabingwa hao watetezi wa La Liga kusajili katika mashindano yote.

Ushindi wa 1-0 dhidi ya Man-United katika mkondo wa pili wa hatua ya 16-bora ya UEFA ugani Old Trafford mnamo Machi 15, ulikuwa wa tatu kwa Atletico kusajili kutokana na mechi nne zilizopita za ugenini. Ni mara ya kwanza tangu 2016-17 kwa Atletico kutinga robo-fainali za UEFA. Chelsea iliwadengua kwenye hatua ya 16-bora kwa mabao 3-0 mnamo 2020-21.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Kibarua akana kuibia KIRDI tarakilishi za Sh150,000

TAHARIRI: Vijana wapaswa kuelimishwa kuhusu hatari ya...

T L