• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 10:08 PM
Man-United kutamatisha mkataba wa Ronaldo kisheria ili aondoke Old Trafford bila ndururu!

Man-United kutamatisha mkataba wa Ronaldo kisheria ili aondoke Old Trafford bila ndururu!

NA MASHIRIKA

MANCHESTER United wamefichua mpango wa kutumia njia mbalimbali za kisheria katika juhudi za kutamatisha mkataba wa nyota Cristiano Ronaldo ugani Old Trafford.

Ilivyo, Ronaldo hawezi tena kuwajibikia mabingwa hao mara 20 wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kutumia mahojiano yake ya hivi majuzi kulipua ‘kibomu’ kuhusu yanayomkera kambini mwa Red Devils.

Sogora huyo raia wa Ureno amesalia na miezi saba pekee katika kandarasi yake ya sasa na Man-United wanaomdumisha kwa mshahara mnono wa Sh72.5 milioni kwa wiki.

Kwa mujibu wa ripoti nyingi nchini Uingereza, Man-United wanawazia kusitisha kanadarasi ya Ronaldo katika hatua itakayomwacha fowadi huyo wa zamani wa Real Madrid na Juventus akiwa huru kuyoyomea anakotaka wakati wa muhula mfupi wa uhamisho wa wachezaji mnamo Januari 2023.

Inafahamika kuwa Man-United hawako radhi kumpokeza Ronaldo fidia au malipo yoyote kutokana na jinsi wanavyohisi kuhusu madai ya mvamizi huyo. Miamba hao wanataka kushughulikia suala la Ronaldo haraka iwezekanavyo ili kuepuka athari za madai na mienendo yake kuvuruga mipango yao ya nusu ya pili ya msimu huu wa 2022-23.

Kocha wa Manchester United Erik ten Hag (kushoto) amwelekeza mshambuliaji Cristiano Ronaldo wakati wa mechi yao dhidi ya Southampton katika uwanja wa St Mary’s mjini Southampton, mnamo Agosti 27, 2022. PICHA | AFP

Katika mahojiano yake, Ronaldo, 37, alidai “kusalitiwa” na waajiri wake Man-United na akafichua kwamba hana heshima kabisa kwa mkufunzi Ten Hag ambaye “ni miongoni mwa vinara watatu wakuu wanaomsukuma nje ya Old Trafford”.

Alikerwa pia na hatua ya Man-United “kutomuonea huruma wala kusimama naye” mwanawe mmoja alipoaga dunia mnamo Aprili kabla ya mwingine mdogo kuugua na kulazwa hospitalini mwezi Julai.

Mnamo Agosti, Mreno huyo aliahidi kuanika anachokipitia kambini mwa Man-United baada ya jaribio lake kuondoka Old Trafford ili apate fursa ya kuchezea kikosi kinachoshiriki soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu kugonga ukuta. Aidha, alifichua kuwa alitupilia mbali ofa ya Sh44 bilioni ili kujiunga na klabu moja ya Saudi Arabia.

Katika taarifa yao ya Novemba 19, Man-United walikiri “kuanzisha mchakato na hatua zinazostahili kukabili madai ya Ronaldo”.

Nahodha huyo wa Ureno anatarajiwa kutambisha taifa lake kwenye fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar na ataelekezewa macho ya karibu wakati wa mchuano wa ufunguzi wa Kundi H dhidi ya Qatar mnamo Alhamisi.

Man-United walipepeta Fulham 2-1 katika gozi la EPL mnamo Jumapili ugani Craven Cottage na kusalia katika nafasi ya tano jedwalini kwa alama 26. Wameshinda mechi nane, kupiga sare mbili na kupoteza michuano minne kati ya 14 ya muhula huu chini ya Ten Hag aliyetokea Ajax ya Uholanzi msimu jana.

Kutokana na ugonjwa ambao haujabainishwa, Ronaldo hajachezea waajiri wake tangu wapigwe 3-1 na Aston Villa mnamo Novemba 6 katika pambano la EPL lililomshuhudia akivalia utepe wa nahodha.

Ten Hag alimwacha Ronaldo nje ya kikosi kilichovaana na Chelsea mwezi uliopita, siku tatu baada ya kukataa kutokea benchi na kucheza dhidi ya Tottenham Hotspur.

“Simheshimu Ten Hag kwa sababu ananidharau. Suala la heshima ni la nipe nikupe,” akasema Ronaldo aliyerejea Man-United mwanzoni mwa msimu wa 2021-22 baada ya kuagana na Juventus waliomsajili kutoka Real kwa mkataba wa miaka minne.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Ghana ndicho kikosi cha wanasoka...

Waendeshaji wa baiskeli 1,000 kushiriki Jubilee Live Free...

T L