• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:55 AM
Man-United wafungulia mifereji ya fedha na kumsajili Casemiro kwa Sh8.4 bilioni kutoka Real Madrid

Man-United wafungulia mifereji ya fedha na kumsajili Casemiro kwa Sh8.4 bilioni kutoka Real Madrid

Na MASHIRIKA

MANCHESTER United wameafikiana na Real Madrid kuhusu uhamisho wa kiungo matata wa Brazil, Casemiro, hadi uwanjani Old Trafford kwa kima cha Sh8.4 bilioni.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 30 amekuwa akivalia jezi za Real tangu mwaka wa 2013 na akasaidia miamba hao kunyanyua mataji matatu ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga) na matano ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Casemiro anatarajiwa kutia saini mkataba wa miaka minne huku akiwa huru kurefusha kandarasi hiyo kwa miezi 12 zaidi kambini mwa Man-United wanaonolewa na kocha Erik ten Hag.

Man-United kwa sasa wanavuta mkia kwenye jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kupoteza mechi mbili za kwanza msimu huu. Mabingwa hao mara 20 wa EPL walipigwa 2-1 na Brighton kabla ya Brentford kuwaponda 4-0. Wana kibarua kigumu cha kujinyanyua dhidi ya Liverpool ligini mnamo Agosti 22, 2022 ugani Old Trafford.

Casemiro anatarajiwa kuwa miongoni mwa wanasoka wanaodumishwa kwa mshahara wa juu zaidi kambini mwa Man-United na atakuwa sogora wa nne kusajiliwa na kikosi hicho muhula huu baada ya kiungo Christian Eriksen na mabeki Tyrell Malacia na Lisandro Martinez.

Man-United walianza kuhemea maarifa ya Casemiro baada ya juhudi zao za kumsajili kiungo mzoefu raia wa Ufaransa, Adrien Rabiot kutoka Juventus kugonga mwamba. Kusajiliwa kwa Casemiro kunatamatisha rasmi pia mbio za Man-United kujinasia huduma za kiungo wa Barcelona, Frenkie de Jong, ambaye sasa anawaniwa na Chelsea.

Casemiro aliwahi kuhudumu kambini mwa FC Porto kwa mkopo mnamo 2014-15 kabla ya kurejea ugani Santiago Bernabeu. Amechezea Real jumla ya michuano 222 na kufunga mabao 24.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Uhaba wa unga bado wasumbua mamilioni

Napoli wajinasia huduma za Tanguy Ndombele kutoka Tottenham

T L