• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Manchester City wazamisha chombo cha Leicester ugenini

Manchester City wazamisha chombo cha Leicester ugenini

Na MASHIRIKA

MABINGWA watetezi Manchester City walisajili ushindi wa tatu mfululizo katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kupokeza Leicester City kichapo cha 1-0 uwanjani King Power.

Makipa Kasper Scheichel na Ederson Moraes walifanya kazi ya ziada kuhakikisha kwamba vikosi vyao vinasalia nguvu sawa hadi dakika ya 62 ambapo Bernardo Silva alizamisha chombo cha wenyeji wao.

Kiungo huyo mvamizi raia wa Ureno alicheka na nyavu za Leicester baada ya kombora lililovurumishwa na Joao Cancelo kumbabatiza beki Caglar Soyuncu na mpira kuangukia kwenye njia ya Silva.

Mambo yakiwa 0-0, Ederson wa Man-City alipangua makombora mawili mazito kutoka kwa Harvey Barnes huku Gabriel Jesus naye akimshughulisha vilivyo Schmeichel.

Leicester walipata nafasi nyingi za wazi kupitia Barnes huku bao la Jamie Vardy likikosa kuhesabiwa kwa madai kwamba alikuwa ameotea.

Bao la Silva linamaanisha kwamba Man-City kwa sasa wameshinda mechi zao zote tatu zilizopita tangu wafungue kampeni za msimu huu wa 2021-22 kwa kichapo cha 1-0 kutoka kwa Tottenham Hotspur.

Chini ya kocha Pep Guardiola, Man-City walimsajili kiungo raia wa Uingereza, Jack Grealish kutoka Aston Villa kwa kima cha Sh15.6 bilioni msimu huu.

Hata hivyo, juhudi zao za kujinasia maarifa ya fowadi Harry Kane kutoka Spurs ziliambulia pakavu.

Kwa kushinda mechi yao ya kwanza ugenini tangu Mei 14, 2021, Guardiola anaamini kwamba masogora wake wamepata motisha ya kutosha kadri wanavyojiandaa kuvaana na RB Leipzig katika mchuano wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Septemba 15, 2021 ugani Etihad.

Kwa upande wao, Leicester ambao sasa wameshinda mechi mbili na kupoteza mbili nyinginezo kati ya nne zilizopita ligini, wamepangiwa kumenyana na Napoli ya Italia mnamo Septemba 16, 2021 katika gozi la Europa League.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Ronaldo afunga mabao mawili Man-U ikicheza dhidi ya...

Walimu 3 waliohitimu PhD wafunza katika chekechea, Gredi ya...