• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Ronaldo afunga mabao mawili Man-U ikicheza dhidi ya Newcastle katika mchezo wake wa kwanza tangu arejee Old Trafford

Ronaldo afunga mabao mawili Man-U ikicheza dhidi ya Newcastle katika mchezo wake wa kwanza tangu arejee Old Trafford

Na MASHIRIKA

CRISTIANO Ronaldo alifunga mabao mawili katika mchuano wake wa kwanza tangu arejee kambini mwa Manchester United na kusaidia mabingwa hao mara 20 wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kupepeta Newcastle United 4-1 ugani Old Trafford.

Akishangiliwa pindi aliposhuka kwenye basi la kikosi chao hadi aliposhiriki mazoezi kabla ya mechi, Ronaldo alisisimua mashabiki kila alipogusa mpira uwanjani na akajibu ushabiki huo mkubwa kwa mabao mawili muhimu.

Miaka 12 tangu afungie Man-United bao lake la mwisho ugani Old Trafford, Ronaldo alifungulia waajiri wake ukurasa wa mabao mwishoni mwa kipindi cha kwanza baada ya kipa Freddie Woodman kutema mpira alioelekezwa na Mason Greenwood.

Baada ya Javier Manquillo ambaye ni beki wa zamani wa Liverpool kusawazishia Newcastle, Ronaldo alishirikiana na Luke Shaw na kufunga bao la pili la Man-United katika dakika ya 62.

Bruno Fernandes ambaye ni mwenzake katika timu taifa ya Ureno alipachika wavuni bao la tatu la kikosi cha kocha Ole Gunnar Solskjaer baada ya kuandaliwa krosi na kiungo Paul Pogba katika dakika ya 80. Jesse Lingard aliyetokea benchi katika kipindi cha pili alizamisha kabisa chombo cha Newcastle United sekunde chache kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mchezo kupulizwa.

Ushindi huo ulipaisha Man-United hadi nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa jedwali la EPL kwa alama 10, moja zaidi kuliko Manchester City, Brighton na Tottenham Hotspur.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Crystal Palace yapiga Spurs breki kali katika EPL

Manchester City wazamisha chombo cha Leicester ugenini