• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 8:50 AM
Manchester City yalipiza kisasi dhidi ya Chelsea ligini

Manchester City yalipiza kisasi dhidi ya Chelsea ligini

Na MASHIRIKA

AZMA ya Chelsea kuendeleza rekodi nzuri ya kutoshindwa katika mechi sita mfululizo za ufunguzi wa kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu ilipigwa breki kali hapo jana na Manchester City.

Chini ya kocha Pep Guardiola, mabingwa watetezi wa EPL Man-City walilipiza kisasi dhidi ya Chelsea kwa kuwapokeza kichapo cha 1-0 ugani Stamford Bridge.

Man-City waliotamalaki mchezo kuanzia dakika ya kwanza hadi mwisho walipoteza nafasi nyingi za wazi kabla ya kombora la Gabriel Jesus kumbabatiza kiungo Jorge Jorginho Frello katika dakika ya 53. Kikosi hicho kiliingia ugani kikilenga kujinyanyua baada ya chombo chao kuzamishwa na Chelsea mara tatu mfululizo mnamo 2020-21.

Fowadi Romelu Lukaku alidhani alikuwa amesawazishia Chelsea ya kocha Thomas Tuchel katika 68 ila bao lake likakosa kuhesabiwa kwa madai kuwa alikuwa ameotea.

Ushindi wa Man-City unamfanya Guardiola ambaye ni raia wa Uhispania kuwa kocha anayejivunia mafanikio makubwa zaidi katika historia ya kikosi hicho ikizingatiwa idadi ya mechi ambazo amesaidia waajiri wake kushinda.

Kabla ya kuongoza Man-City kupepetana na Chelsea, kocha huyo wa zamani wa Barcelona na Bayern Munich alikuwa amesaidia waajiri wake wa sasa kushinda mechi 220 sawa na mkufunzi nguli wa kikosi hicho, Les McDowall.

Huku McDowall akifikia rekodi hiyo baada ya kusimamia mechi 592, Guardiola alihitaji michuano 302 pekee, 38 chini ya mapambano ambayo aliyekuwa kocha wa Man-City, Joe Mercer aliwahi kuhitaji.

“Rekodi hii ni ufanisi mkubwa. Imekuja kwa wakati ufaao na itatuchochea kujitahidi hata zaidi katika mashindano yajayo,” akasema Guardiola, 50.

Kufikia sasa, Guardiola ndiye mkufunzi anayeshikilia rekodi ya kushindia Man-City idadi kubwa zaidi ya mataji kuliko kocha yeyote mwingine katika historia ya kikosi hicho.

Mataji manane ya haiba kubwa ambayo amezolea miamba hao ni maradufu ya kiasi ambacho nambari mbili Mercer alinyanyulia Man-City. McDowall aliyekuwa mkufunzi wa Man-City kati ya 1950 na 1963 alishindia kikosi hicho Kombe la FA pekee mnamo 1956.

Baada ya kumenyana jana na Chelsea, Man-City kwa sasa wanajiandaa kuvaana na Paris Saint-Germain (PSG) ya Ufaransa katika Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) mnamo Jumanne ijayo kabla ya kushuka dimbani kupepetana na Liverpool katika EPL ugani Anfield.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

FATAKI: Komesheni tabia ya kutia mkono chunguni kabla mboga...

Alaves wakomesha rekodi nzuri ya Atletico Madrid kwenye La...