• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 6:50 AM
Manchester United wapiga Arsenal breki kali EPL

Manchester United wapiga Arsenal breki kali EPL

Na MASHIRIKA

SAJILI mpya wa Manchester United, Antony dos Santos alifunga bao katika mchuano wake wa kwanza kambini mwa miamba hao na kusaidia kikosi hicho kupepeta Arsenal 3-1 katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ugani Old Trafford.

Ushindi huo wa Man-United wanaonolewa na kocha Erik ten Hag ulipiga breki mwanzo bora wa Arsenal waliokuwa wametamalaki mechi sita zote sita za ufunguzi wa EPL msimu huu.

Antony aliyesajiliwa na Man-United kwa Sh11.6 bilioni kutoka Ajax ya Uholanzi, alifungulia waajiri wake ukurasa wa mabao katika dakika ya 35 kabla ya Bukayo Saka kusawazisha mambo katika dakika ya 60.

Magoli mengine ya Man-United yalijazwa kimiani na Marcus Rashford katika dakika ya 66 na 75 mtawalia. Mabao hayo yalichangiwa na kiungo mbunifu raia wa Ureno, Bruno Fernandes aliyeshirikiana vilivyo na Christian Eriksen.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa Rashford kufunga mabao mawili katika mchuano mmoja wa EPL tangu Disemba 2020. Man-United ambao ni mabingwa mara 20 wa EPL sasa wanakamata nafasi ya tano jedwalini kwa alama 12, tatu pekee nyuma ya Arsenal wanaoselelea kileleni.

Arsenal walishuka dimbani wakilenga kushinda mechi sita mfululizo mwanzoni mwa msimu kwa mara ya kwanza tangu 1947. Hata hivyo, walizidiwa ujanja na wenyeji wao waliotamalaki mchezo katika safu ya kati huku nahodha Martin Odegaard akizidiwa maarifa na Eriksen.

Kupigwa kwa Arsenal huenda kukawa mwanzo wa kushuka kwa makali yao ambayo yatatiwa kwenye mizani zaidi watakapokutana na Tottenham Hotspur, Liverpool na Manchester City kwa usanjari huo mnamo Oktoba 2022.

Kabla ya hapo, Arsenal watavaana na FC Zurich ya Uswsi kwenye Europa League mnamo Septemba 8, 2022 kisha kushuka ugani Everton na PSV Eindhoven ya Uholanzi. Watafunga kampeni za Septemba 2022 kwa kumenyana na Brentford ligini kisha kufungua Oktoba kwa gozi kali la EPL dhidi ya Spurs.

Man-United wataanza kampeni za Oktoba 2022 kwa kibarua kizito dhidi ya Manchester City ugani Etihad baada ya kuchuana na Real Sociedad na Sheriff Tiraspol kwenye Europa League na kukwaruzana na Palace na Leeds United ligini.

Arsenal sasa wameshinda Man-United mara moja pekee kutokana na mechi 16 zilizopita za EPL ugani Old Trafford.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Kiraitu sasa adai Munya ndiye alichangia kushindwa kwake na...

Mbappe na Messi watambisha PSG dhidi ya Nantes katika...

T L