• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 10:15 PM
Mane amfuata Ronaldo nchini Saudi Arabia

Mane amfuata Ronaldo nchini Saudi Arabia

NA MASHIRIKA

MUNICH, Ujerumani

MSHAMBULIAJI Sadio Mane ameagana na klabu ya FC Bayern Munich ya Ujerumani na kujiunga na Al Nassr ya Ligi Kuu nchini Saudi Arabia, kuungana na mkali mwenzake Cristiano Ronaldo.

Staa huyo wa kimataifa wa Senegal mwenye umri wa miaka 31 alikuwa na maisha magumu pale Allianz Arena kiasi cha kuamua kondoka ili kuanza maisha mapya Mashariki ya Kati.

Straika huyo aliyejiunga na Munich akitokea Liverpool mwaka uliopita amesajiliwa kwa Sh6.3 bilioni kiasi kilichotumika kumnunua.

Akiwa na Bayern Munich, Mane alicheza mechi 38 katika mashindano tofauti, huku akifunga mabao 12 na kuisaidia klabu hiyo kutwaa ubingwa wa Bundesliga wa msimu wa 2022/2023.

Al Nassr imeamua kukisuka kikosi kwa kuleta vifaa kadhaa matata baada ya kuambulia patupu kushinda chochote msimu uliopita.

Mbali na Mane na Ronaldo, klabu hiyo kadhalika ilifanikiwa kuwanasa Marcelo Brozovic kutoka Inter Milan, Seko Fofana kutoka Lens na Alex Telles aliyetoka Manchester United.

Vile vile klabu hiyo imesajili Anderson Talisca na kipa wa zamani wa Arsenal, David Ospina, huku malengo yakiwa kushinda ubingwa wa ligi kuu ya Saudi Arabia baada ya kumaliza katika nafasi ya pili, nyuma ya Al-Ittihad kwa tofauti ya pointi tano jedwalini.

Mane aliye na uwezo wa kucheza kama mshambuliaji wa katikati na pia kama winga wa pande zote mbili ameletwa kwa ajili ya kusaidia Ronaldo kuimarisha safu ya ushambuliaji, ambapo ni Ronaldo aliyeongoza kwa ufungaji mabao alipopachika wavuni mabao 14.

Mbali na kuvurugwa na jeraha lililomfanya akose nafasi katika kikosi cha Senegal kilichoshiriki fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar, Mane pia alipigwa marufuku kwa muda baada ya kumpiga kiwiko mwenzake Leroy Sane walipokuwa wakicheza dhidi ya Manchester City katika pambano la Klabu Bingwa.

Afisa Mkuu wa Bayern Munich, Jan Christian Dreesen alisema nyota huyo wa zamani wa Southampton amesajiliwa na Al Nassr kwa mkataba wa miaka minne.

Kocha Thomas Tuchel alisema walikubaliana staa huyo aondoke baada ya kuendelea kupata upinzani mkali kikosini.

  • Tags

You can share this post!

Waitaliano wasitozwe ada ya Visa – mbunge

Serikali ya sarakasi

T L