• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:46 PM
Waitaliano wasitozwe ada ya Visa – mbunge

Waitaliano wasitozwe ada ya Visa – mbunge

NA MAUREEN ONGALA

MBUNGE wa Kilifi Kaskazini Owen Baya ameitaka serikali ya Kenya Kwanza inayoongozwa na Rais William Ruto kufutulia mbali pesa wanazotozwa watalii kutoka nchini Italia ili kupata Visa.

Bw Baya alisema kuwa nchi hii inaendelea kupoteza polepole watalii wa Kiitaliano ambao wanazidi kuchoshwa na mchakato mrefu na ghali wa kupata Visa kabla ya kusafari.

Kulingana na Baya, imekuwa changamoto kwa watalii hao kupata cheti hicho ambacho huchukua muda mrefu kutayarsishwa.

Akizungumza katika mahojiano na Taifa Leo, Bw Baya alisema kuwa huku nchi nyingine zikiwapa watalii hao nafasi nzuri ya kutalii kwao, Kenya imebaki kuwapa sheria na masharti magumu hali ambayo inawavunja moyo kila kuchao.

“Kuna Waitaliano wengi ambao wamewekeza katika mji wa Malindi na pia mji wa Watamu lakini lakini biashara hizo zimekufa kwa sababu watalii wanahamia visiwani Zanzibar, Maldives na Ushelisheli kwa sababu asasi za huko zimerahisisha usafiri kuenda kwao,” akasema.

Alisema kuwa nchi hizo zimerahisisha mipango yote ya watalii kusafiri kuzuru huko kwani mtalii anahitaji tu kukata tikiti na kusafiri bali sio Visa.

Bw Baya alisema kuwa Malindi na Watamu hupata takriban watalii 500,000 kila msimu na kwamba idadi hii inaweza ikaongezeka hadi 2 milioni.

Aliongeza kusema ya kwamba Waitaliano wengi wanatambua Kenya kuwa makao yao ya pili na iwapo serikali itafutilia mbali ada wanazotozwa wanapotafuta Visa basi itakuwa hatua itakayoinua sekta ya utalii kwa kuongeza idadi ya watalii na pia kuwavutia wengi wao kuwa wawekezaji.

“Waitaliano wamekuwa wavumilivu sana na nchi yetu imewategemea watalii wa Kiitaliano pakubwa hata wakati Waingereza, Waswisi na Wajerumani walirudi katika mataifa yao, tulibaki na Waitaliano kwa sababu wanapenda nchi yetu sana. Tuko na idadi kubwa ya wawekezaji katika sekta ya utalii ambao ni Waitaliano, “akasema.

 

Bi Elisabetta Bettoni kutoka nchini Italia na ambaye ni mmiliki wa Ocean Beach Resort and SPA iliyoko mjini Malindi. PICHA | MAUREEN ONGALA

Mbunge huyo alisema kuwa Waitaliano waliibua kumbukumbu za kipekee na mji wa Malindi tokea miaka ya sitini yaani 1960s.

Bw Baya alisema kuwa hali ya uwanja wa ndege wa kimataifa wa Malindi imekuwa changamoto kubwa kwa sekta ya utalii kwani hauwezi kutoa Visa kwa watalii.

“Uwanja wa ndege wa Malindi hautoi huduma za kimataifa kwa watalii na hiyo imekuwa changamoto kubwa ya nchi yetu kufikia watalii nchini Italia,” akasema.

Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Malindi. PICHA | MAKTABA

Alisema kuwa ndege za shirika la Kenya Airways haziendi nchini Italia na watalii hulazimika kusafiri kwa mwendo mrefu, safari hiyo ikiwa ya kuchosha kwa sababu wanalazimika kuabiri ndege tofauti wanapotua Nairobi ili iwafikishe mjini Malindi.

“Tunataka kuona utalii wetu unarudia misimu miwili kama hapo awali na tunaweza kufanikisha hili iwapo tutoa mazingira mazuri kwa watalii wa Kiitaliano,” akasema.

Bw Baya pamoja na gavana wa Kilifi Gideon Mung’aro walimtaka Rais Ruto kukamilisha kulipa fidia ya familia kando ya uwanja wa ndege wa Malindi ili kuanzisha mara moja ujenzi wa kupanua uwanja huo.

Ndege ya Skyward Express ikitua katika Uwanja wa Ndege wa Malindi, Kaunti ya Kilifi katika safari ya kwanza kabisa ya ndege za shirika hilo kutoka Nairobi hadi Malindi mnamo Februari 10, 2021. PICHA | KEVIN ODIT

Wito wa viongozi hao wawili unajiri hata baada ya wadau katika sekta ya utalii katika Kaunti ya Kilifi, wakiongozwa na mwenyekiti wa hoteli za Jacaranda mjini Watamu Pasquel Tirito, wakimtaka Rais Ruto kutimiza ahadi alizotoa wakati wa kampeni ambapo alisema ana mpango kabambe wa kuimarisha sekta hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Beldine ndiye kocha wa kike pekee KWPL

Mane amfuata Ronaldo nchini Saudi Arabia

T L