• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:46 PM
Serikali ya sarakasi

Serikali ya sarakasi

NA WANDERI KAMAU

KATIKA muda wa miezi tisa pekee tangu ishike mamlaka, serikali ya Rais William Ruto imejitokeza kama utawala uliokosa dira hasa kuhusu mfumo wa mawasiliano, na mkwaruzano wa kimajukumu miongoni mwa mawaziri.

Ni hali ambayo imewafanya baadhi ya mawaziri kutoa taarifa zinazokanganya, jambo ambalo mara nyingi limewaacha raia kwenye sintofahamu kuhusu msimamo wa serikali kuhusu baadhi ya masuala yenye umuhimu wa kitaifa.

Ijapokuwa mtindo huo umekuwa ukishuhudiwa tangu Rais Ruto aingie madarakani Septemba 2022, mnamo Jumanne, ulionekana kumtia hofu alipokiri kuwa baadhi ya mawaziri hata hawajui mambo yanayoendelea katika wizara zao.

Mawaziri waliojipata katika mgongano wa kimajukumu ni Waziri wa Usalama wa Ndani Kithure Kindiki na mwenzake wa Habari na Mawasiliano (ICT) Eliud Owalo, Waziri wa Biashara Moses Kuria na mwenzake Mithika Linturi wa Kilimo, Dkt Alfred Mutua (Mashauri ya Kigeni), Dkt Susan Nakhumicha (Afya) na Aisha Jumwa (Jinsia na Utumishi wa Umma).

Hapo jana Jumatano, Prof Kindiki alitofautiana vikali na Bw Owalo kuhusu shughuli yenye utata ambapo maelfu ya Wakenya wamekuwa wakisajiliwa katika mradi tata wa sarafu ya kidijitali ya Worldcoin.

Shughuli hiyo ilianza wiki iliyopita, ambapo raia wamekuwa wakijitokeza kusajiliwa, baada ya kubainika aliyesajiliwa hupokea Sh7,000 kwenye akaunti yake.

Katika mahojiano, Bw Owalo alisema kuwa shughuli hiyo ambayo imekuwa ikiendeshwa na kampuni ya kijiditali ya OpenAI kutoka Amerika “inaendeshwa kulingana na sheria”.

“Hii ni shughuli ambayo ilianza Aprili. Tuna afisi ya Kamishna wa Data, yenye jukumu la kusimamia na kulainisha masuala ya usalama wa data za raia. Mnamo Aprili, tuliiandikia barua afisi hiyo na kuifahamisha kuhusu yale kampuni hiyo (OpenAI) ilikuwa ikikusudia kufanya,” akasema Bw Owallo.

Hata hivyo, Prof Kindiki alitangaza kusimamisha mara moja shughuli hiyo, akieleza hofu kuhusu “usalama wa maelezo ya raia yanayochukuliwa”.

“Serikali imesimamisha mara moja shughuli hizo hadi pale taasisi husika za umma zitakapowaidhinisha wale wanaoziendesha. Tutachukua hatua kali dhidi ya yule atakayeshiriki kwa vyovyote vile ama kuwasaidia wahusika,” akasema Prof Kindiki kwenye taarifa.

Muda mfupi baadaye Dkt Mutua aliunga mkono hatua ya Prof Kindiki akisema “Wakenya si panya wa maabara wa kufanyiwa majaribio.”

Novemba 2022, mawaziri Kuria na Linturi walitofautiana vikali kuhusu hatua ya serikali kuagiza magunia milioni 10 ya mahindi ya kisayansi (GMO).

Bw Kuria alisisitiza kuwa serikali ilikuwa tayari imeanza mpango wa kuagiza mahindi hayo, ili kukabili hali ya njaa iliyokuwa ikiendelea nchini.

“Kama Waziri wa Kilimo, sifahamu lolote kuhusu mpango wa serikali kuagiza mahindi ya GMO,” akasema Bw Linturi.

Hata hivyo, Bw Kuria alisisitiza kuwa njia pekee ya serikali kukabili hali ya njaa ilikuwa kuagiza mahindi hayo.

“Tumeamua kuagiza mahindi ya GMO hadi pale tutakapokuwa na chakula cha kutosha,” akasema Bw Kuria.

Jumamosi wiki iliyopita, Waziri Nakhumicha alitoa agizo la kumhamisha Mkuu wa Polisi (OCS) katika eneo la Matisi, Kaunti ya Trans Nzoia, John Thuo, kutokana na “ukosefu wa usalama” katika eneo hilo.

“Tunatumia mfumo wa serikali moja. Hilo linamaanisha kuwa ninaposimama hapa, ninaiwakilisha serikali ya Rais William Ruto. Hivyo basi ninaagiza kuhamishwa kwa OCS wa Matisi. Ikiwa mkuu wa polisi wa Kaunti yuko hapa, aambiwe kuwa Waziri amesema kufikia kesho, mkuu huyo hafai kuwa hapa,” akasema.

Kirasmi jukumu la kuwahamisha wakuu wa polisi ni la ama Inspekta Jenerali wa Pilisi au Waziri wa Usalama.

Mnamo Novemba 2022, Waziri Jumwa alisema kuwa watumishi wa umma wataongezwa mishahara yao kwa muda wa siku 100.

Hii ni licha ya kuwa nyongeza yoyote ya mishahara ya wafanyakazi wa serikali lazima iidhinishwe na Tume ya Utumishi wa Umma (PSC) na Tume ya Mishahara na Marupurupu (SRC).

“Watumishi wa umma hawana motisha na hatutaki kuona wakiteseka. Hawana uwezo wa kukabiliana na gharama ya juu ya maisha iliyosababishwa na mfumuko wa bei. Tunataka kuimarisha motisha yao kwa kuwaongeza mishahara katika siku chache zijazo,” akasema.

Mnamo Mei, Dkt Mutua alisema kuwa serikali ya Kenya imebuni ushirikiano na serikali ya Canada kwa lengo la“kuwasaidia Wakenya kupata kazi nchini humo”.

“Nina furaha kutangaza kwamba kuna nafasi nyingi za kazi katika sekta nyingi nchini Canada na Wakenya wanaweza kusafiri nchini humo kama wanafunzi, watalii au wafanyakazi. Ni mpango ambao tumebuni baina ya serikali hizi mbili.”

Siku moja baadaye, Idara ya Uhamiaji ya Canada ilikanusha kauli yake.

“Kuna habari zinazoenea kwamba kuna mipango maalum inayowakaribisha wahamiaji kutoka Kenya kuzuru Canada. Huo ni uongo, kwani hakuna mpango kama huo,” ikasema idara hiyo.

Mnamo Julai, Bw Kuria alizua hisia kali aliposema kuwa ataenda haja ndogo katika lango la makazi ya Mamake Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta, Mama Ngina Kenyatta “kulalamikia hatua ya Bw Kenyatta kufadhili maandamano ya Azimio la Umoja”.

“Siogopi. Nitaenda haja ndogo katika lango la makazi yake na sitaogopa. Lazima (familia ya Kenyatta) iache kusumbua nchi,” akasema akiwa Ruiru, Kiambu.

Kutokana na matamshi hayo, wadadisi wanasema kuwa tatizo kuu lililopo ni ukosefu wa mfumo maalumu wa mawasiliano katika serikali.

“Migongano hii ya kauli inadhihirisha ukosefu wa mawasiliano kuhusu msimamo wa serikali kwa masuala yenye uhumimu . Inatoa taswira ya yanayojiri katika vikao vya Baraza la Mawaziri,” asema mdadisi wa siasa Kipkorir Mutai.

Mdadisi huyo anaeleza kuwa Rais Ruto anafaa kubuni mfumo thabiti wa mawasiliano, ili kuepuka migongano kama hiyo, kwani inaathiri sana sifa ya serikali yake

  • Tags

You can share this post!

Mane amfuata Ronaldo nchini Saudi Arabia

Wafanyakazi kuanza kukatwa ushuru wa nyumba

T L