• Nairobi
  • Last Updated May 3rd, 2024 3:16 PM
Mbappe avunja rekodi ya ufungaji mabao katika soka ya Ligi Kuu ya Ufaransa

Mbappe avunja rekodi ya ufungaji mabao katika soka ya Ligi Kuu ya Ufaransa

Na CHRIS ADUNGO

MFUMAJI chipukizi Kylian Mbappe alicheka na nyavu mara mbili na kuongoza Paris Saint-Germain (PSG) kusajili ushindi wa 4-2 dhidi ya Olympique Lyon katika Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1) mnamo Jumapili usiku.

Ushindi huo wa PSG wanaotiwa makali na kocha Mauricio Pochettino, uliwasaidia kutua kileleni mwa jedwali la Ligue 1 kwa alama 63 sawa na Lille waliopokezwa kichapo cha 2-1 kutoka kwa Nimes.

Mbappe, 22, sasa anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji mchanga zaidi kuwahi kufunga jumla ya mabao 100 katika soka ya Ligue 1.

Mbappe alifungulia PSG ukurasa wa mabao katika dakika ya 15 kabla ya Danilo Pereira kuongeza la pili kunako dakika ya 32 kisha Angel Di Maria akapachika wavuni la tatu mwanzoni mwa kipindi cha pili.

Mbappe alifunga tena katika dakika ya 52 kabla ya mapigo hayo ya PSG kujibiwa kwa mabao kutoka kwa Islam Slimani na Maxwel Cornet katika dakika za 62 na 81 mtawalia.

Ushindi kwa PSG unaweka pazuri kuhifadhi taji la Ligue 1 msimu huu baada ya presha ya kusalia kileleni mwa jedwali kuwalemea washindani wakuu hasa Lille waliozamishwa na Nimes 2-1 huku Lyon wakisalia katika nafasi ya tatu kwa pointi 60.

Mbappe kwa sasa ameivunja rekodi ya Herve Revelli aliyefunga jumla ya mabao 100 akivalia jezi za Saint Etienne mnamo 1969 na kuwa mwanasoka mchanga zaidi kuwahi kufikisha magoli 100 katika soka ya Ligi Kuu ya Ufaransa.

Mechi hiyo ilikuwa pia fursa mwafaka kwa PSG kumkaribisha kikosini fowadi matata raia wa Brazil, Neymar Jr ambaye amekuwa mkekani kwa wiki sita zilizopita kuuguza jeraha. Neymar aliingia uwanjani katika dakika ya 70 kujaza pengo la Mbappe katika mchuano huo dhidi ya Lyon.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Harambee Stars, Mafirauni waingia kambini kabla ya kukabana...

Chiefs yakaribisha Mkenya Teddy Akumu ikirarua Orlando...