• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 10:50 AM
Mbungo kupanga upya mikakati ya kuinoa timu yake ya Bandari FC

Mbungo kupanga upya mikakati ya kuinoa timu yake ya Bandari FC

Na ABDULRAHMAN SHERIFF

YALE aliyopanga kuyatekeleza kocha wa Bandari FC Andre Cassa Mbungo yalitibuka pale mechi za Ligi Kuu ya Betking zilisimamishwa kwa sababu ya kuzuia maambukizo ya virusi vya corona.

Mbungo alisema Alhamisi kuwa alipanga mikakati mizuri ya timu yake hiyo yenye makao makuu Pwani kufanya vizuri kwenye ligi hiyo na wamekuwa wakishinda, lakini ziliposimamishwa mechi, amelazimika apange upya mipango itakayoifanya timu iendelee kushinda mechi zake.

“Mechi zilipositishwa zilinitibulia mipango yangu kwani tulikuwa tukiendelea vizuri na nilikuwa sina shaka tungekamilisha ligi katika nafasi mojawapo ya tatu za mwanzo,” akasema Mbungo huku akipanga mikakati mingine ya kufanya vizuri katika mechi zilizobakia.

Alisema timu yake ilikuwa ikiwika na kwa mipango aliyokuwa akiyatekeleza, Bandari ilendelea kufanya vizuri katika ligi hiyo na hata pale walipofanikiwa kuibuka timu bora ya mwezi Februari.

Mbungo anasema mbali na kukosa kutekeleza mipango yake kutokana na sababu hiyo, aliahidi kujitahidi kuhakikisha timu yake inafanya vizuri lakini hakuwa tayari kuahidi kuibuka washindi kwa sababu kwa kipindi cha zaidi ya mwezi mmoja, wachezaji wake hawakufanya mazoezi.

“Japo niliwasihi wanasoka wangu wafanye mazoezi ya kibinafsi, sijui uhakika walivyo mpaka watakapokutana na kuanza mazoezi ya pamoja. Kwa kuwa sisi ni timu inayodhaminiwa na shirika la serikali, tuliwajibika kufuata kikamilifu kanuni za kujikinga na corona.

“Nina hakika ziko timu ambazo zilikuwa zikifanya mazoezi kwa kujificha lakini sisi hatukuweza kufanya hivyo kwa sababu tunahusika na serikali na hatufai kukiuka masharti yaliyowekwa,” akasema Mbungo.

Anasema atajitahidi kuhakikisha ile fomu ya wachezaji wake waliyokuwa nayo kabla ya mechi kusimamishwa, inarudi ili wakamilishe mechi zao zilizobakia kupata ushindi na kumaliza ligi katika nafasi nzuri.

Mbungo anasema anasubiri kwa hamu kuanza kwa mazoezi ya pamoja ya wachezaji wake ambapo watazingatia masharti yatakayowekwa na wizara za afya na michezo, ili aweze kuwanoa na waweze kurudia hali zao walizokuwa nazo hapo awali.

Kuhusu wachezaji wake, Mbungo alisema wanasubiri kwa hamu kuanza mazoezi ya pamoja huku akithibitisha kuwa golikipa wake raia wa Burundi, Justin Ndikumana ameshawasili Mombasa.

“Ndikumana yuko Mombasa na yuko tayari kuanza mazoezi kutoka kwa kocha wa magolikipa Wilson Obungu akiwa na wenzake mara tutakapopewa ruhusa ya kuanza mazoezi ya pamoja,” akasema.

You can share this post!

Bunge la Kitaifa lapitisha Mswada wa BBI

Idd-ul-Fitr: Serikali yatangaza Mei 14 ni siku ya mapumziko