• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 5:50 AM
McGrath ajumuisha Injera kikosi cha Kombe la Dunia 2022

McGrath ajumuisha Injera kikosi cha Kombe la Dunia 2022

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA mkuu Damian McGrath ameita tena wachezaji saba wazoefu na kuwapa fursa watano wapya katika kikosi cha Kenya Shujaa kitakachoshiriki Kombe la Dunia mjini Cape Town, Afrika Kusini mnamo Septemba 9-11.

Mfungaji wa zamani wa miguso mingi kwenye Raga za Dunia, Collins Injera yuko mbioni kushiriki kombe la nne la dunia baada ya 2009, 2013 na 2018, na ataungana na William Ambaka na Billy Odhiambo (tatu kila mmoja) nao nahodha Nelson Oyoo, Samuel Oliech, Jeff Oluoch na Herman Humwa watashiriki kwa mara ya pili.

Johnstone Olindi, Vincent Onyala, Kevin Wekesa, Tony Omondi na Edmund Anya watashiriki Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza kabisa.

Akizungumzia kikosi alichochagua, McGrath alisema, “Tumeshuhudia wachezaji kadha wakijiondoa wenyewe. Hatutakuwa na Alvin Otieno ambaye ameojiondoa katika mpango wa timu ya Shujaa kwa sababu za kibinafsi…ni pigo kubwa kwa sababu ni mmoja wa mafowadi wazuri duniani katika raga ya wachezaji saba kila upande. Tumewapoteza pia Daniel Taabu na Bush Mwale kwa sababu za kinidhamu ambazo zimetatuliwa, lakini ilitulazimu tuwaache nje kwanza. Ni pigo, lakini tuna imani na kikosi tulichochagua,” alisema Mwingereza huyo.

Kuhusu kurejea kwa Injera, McGrath alisema, “Collins analeta uzoefu mkubwa. Ameishi raga na kuifanya, hakuna wachezaji wengi katika Raga za Dunia ambao wamefanya kile Collins amefanikiwa kufanya, ushawishi wake mazoezini ni mzuri sana. Ni mzuri sana na wachezaji chipukizi na anaelewa jinsi raga ya wachezaji saba kila upande inafaa kuchezwa. Kufuatia kujiondoa kwa wachezaji kadha tumekuwa nao, tulihisi kuwa ni vyema kujumuisha mtu kama Collins kuleta ujuzi alionao timuni.”

Shujaa inaelekea katika Kombe la Dunia kwa mara ya sita mfululizo tangu ifuzu mara ya kwanza 2001. Itaanza kampeni dhidi ya Tonga.

Kikosi cha Kenya Shujaa: Nelson Oyoo (nahodha), Collins Injera, Billy Odhiambo, William Ambaka, Samuel Oliech, Herman Humwa, Jeff Oluoch, Johnstone Olindi, Anthony Omondi, Vincent Onyala na Kevin Wekesa na Edmund Anya.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Nambari mpya za usajili wa magari zina manufaa...

Kamket atangaza kushirikiana na Kenya Kwanza

T L