• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 6:55 AM
Messi ateua kuhamia Amerika kuchezea Inter Miami licha ya ofa nono kutoka Al-Hilal ya Saudi Arabia

Messi ateua kuhamia Amerika kuchezea Inter Miami licha ya ofa nono kutoka Al-Hilal ya Saudi Arabia

Na MASHIRIKA

NGULI wa timu ya taifa ya Argentina, Lionel Messi, atajiunga na kikosi cha Inter Miami nchini Amerika baada ya kuagana na miamba wa Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1), Paris Saint-Germain (PSG).

Messi, 35, alikuwa na ofa nono zaidi ya kusajiliwa na kikosi cha Al-Hilal kinachoshiriki Ligi Kuu ya Saudi Arabia baada ya uwezekano wake wa kurejea Barcelona kupata kizingiti cha kanuni za matumizi ya fedha (FFP).

“Nimefikia uamuzi wa kuondoka bara Ulaya na kuyoyomea Miami,” Messi akaambia magazeti ya Diario Sport na Mundo Deportivo.

“Ni ukweli kwamba nilikuwa na ofa kadhaa kutoka kwa kikosi kingine cha bara Ulaya. Hata hivyo, sikufikiria hata kidogo kuhusu ofa hiyo kwa sababu klabu ya pekee ambayo ningejiunga nayo Ulaya ni Barcelona,” akasema.

“Baada ya kushinda Kombe la Dunia na kuzuiwa kurejea Barcelona, sasa ni wakati wa kuonja uhondo wa Major League Soccer (MLS), kucheza soka katika mazingira mengine kwa namna nyingine tofauti na kufurahia maisha yangu siku baada ya nyingine,” akaongezea.

“Bila shaka malengo ni yale yale ya kucheza kwa ajili ya kushinda mataji zaidi. Hata hivyo, tofauti ni kwamba nitakuwa na fursa ya kufanya hivyo bila makeke mengi,” akaelezea fowadi huyo aliyeagana na Barcelona mnamo 2021 na kuyoyomea PSG.

Kwa kuteua kuhamia Miami, Messi ambaye atacheza soka kwa mara ya kwanza nje ya bara Ulaya, atapata fursa tele za kibiashara ikiwemo ushirikiano na Adidas pamoja na Apple.

Sogora huyo tayari ni mshindi mara saba wa Ballon d’Or na anatarajiwa kunyanyua taji hilo kwa mara nyingine baadaye mwaka huu baada ya kuongoza Argentina kushinda Kombe la Dunia mnamo 2022 nchini Qatar.

Messi tayari anamiliki nyumba Miami na amekuwa akiikodisha. Japo aliongoza PSG kushinda mataji mawili ya Ligue 1, mchango wake kisoka nchini Ufaransa haukuhisika pakubwa baada ya waajiri wake kuaga kipute cha Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) katika hatua ya 16-bora.

Alipachika wavuni mabao 32 kutokana na mechi 75 na akakamilisha kampeni za msimu huu wa 2022-23 na mabao 16 huku akichangia 16 mengine.

Aliondoka Barcelona mnamo 2021 baada ya kuwasakatia kwa kipindi cha miaka 21 ambapo aliibuka mfungaji bora wa muda wote kwa mabao 672 huku akinyanyua mataji 10 ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), manne ya UEFA na saba ya Spanish Cup.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Naibu Rais: Nimeokoka na majina yangu kamili ni Geoffrey...

Kitendawili cha kifo cha Jeff Mwathi kuteguliwa kuanzia...

T L