• Nairobi
  • Last Updated April 26th, 2024 7:00 PM
Mogotio United yazidi kung’aa

Mogotio United yazidi kung’aa

NA RICHARD MAOSI

KIKOSI cha Mogotio United kinajivunia wachezaji mahiri ambao wanasakata soka katika kiwango cha Kaunti ya Baringo baadhi yao wakilenga kujiunga na Harambee Stars.

Mkufunzi Bethwel Kipkoech anasema licha ya kikosi chake kutokea mashinani, wanajizatiti kuendeleza wimbi la mashindano makali dhidi ya mahasimu zao ligini.

Licha ya kushiriki michuano ya kirafiki, wanajituma, kuweka timu yao pazuri wakiamini kuwa siku za mbeleni watakuja kushiriki kwenye Ligi ya Kitaifa(KPL).

Akizungumza na Taifa Leo, Bethwel anasema baadhi ya wachezaji wake wamepata fursa ya kushiriki kwenye majaribio ya kujiunga na timu ya Harambe Stars.

Aidha anasema timu za mashinani ndizo hukuza wachezaji mahiri, kama vile Michael Olunga na Victor Wanyama ambao wanacheza soka ya kulipwa kwenye rubaa za kimataifa.

Mmoja wao ni Jazir Hamza kijana wa miaka 14, ambaye alifanya vyema kwenye majaribio ya kujiunga na kikosi cha U-16 , ingawa hangemudu kutokana na umri mdogo.

Alieleza kuwa ni fahari kila mara anapowaona wachezaji wake wakifanya vyema kwenye rubaa mbalimbali, licha ya kufunga magoli mengi na kutandaza kabumbu safi.

Anasema kuwa mafanikio ya wachezaji wa soka mashinani hayajaimarika sana ikilinganishwa na timu zinazoshiriki kabumbu mjini.

“Hii ikitokana na ukosefu wa miundo misingi ya kutosha na uzoefu wa kiwango cha juu kwa wakufunzi,”akasema.

Hata hivyo anaamini kuwa endapo kaunti itaendelea kuwekeza kwa vipaji vya vijana ambao wanatokea mashinani, bila shaka jambo hili litasaidia kuziba nakisi ya wachezaji baina ya vikosi vya soka mashinani.

Kikosi cha Mogotio United chini ya ukufunzi wake kimeendelea kuandikisha matokeo mazuri kwa kushiriki ligi mbalimbali kma vile Sialo Sevens Aside, ligi ya kaunti na ile ya divisheni ya pili.

Aidha baadhi ya wachezaji wamekuwa wakipata ufadhili wa kujiunga na shule ambazo zinalea na kukuza talanta hususan shule ya Upili ya Musingu katika mkoa wa Magharibi.

Mkufunzi Betwel anasema ili kuhakikisha wachezaji wake wanaonyesha mchezo mzuri anahakikisha wanafanya mazoezi ya kutosha mbali na kusakata mechi nyingi za kirafiki kujipima nguvu.

Licha ya kukosa uwanja wa kisasa wa kufanyia mazoezi kwa timu nyingi za mashinani, hii haimaanishi kuwa imezima ndoto zao kupiga hatua katika kandanda.

Nahonda wa kikosi cha Mogotio United Hamza Jazir anasema ushirikiano na bidii za wachezaji ndio uti wa mgongo kwa mafanikio ya timu yao ambayo inaendelea kung’aa Baringo.

You can share this post!

BBI: Reggae yazimwa kwa mara ya tatu

Dortmund wacharaza RB Leipzig na kutia kapuni taji la...