• Nairobi
  • Last Updated April 27th, 2024 4:54 PM
Mombasa yasitisha mashindano ya ndondi hadi michezo ya Olimpiki itakapotamatika

Mombasa yasitisha mashindano ya ndondi hadi michezo ya Olimpiki itakapotamatika

Na CHARLES ONGADI

SHIRIKISHO la Ndondi Nchini (BFK) tawi la Mombasa, limesitisha shughuli zake zote hadi kumalizika kwa Michezo ya Olimpiki ya Tokyo nchini Japan.

Lemy ‘Cobra’ Katibi ambaye ni mpanga ratiba wa ndondi Mombasa, amesema mashindano yote yaliyoratibiwa kufanyika Julai yamesitishwa hadi timu ya taifa ‘Hit Squad’ itakaporudi kutoka Japan.

Katibi ambaye amewahi kuwa kocha wa klabu ya Shirika la Posta na Simu iliyong’ara sana miaka ya 80 na 90 kabla ya kusambaratika, ameziomba klabu kujiandaa kwa mashindano ya chipukizi ya novices.

Awali Mombasa iliratibu kuanza mashindano yake mwezi uliopita ila tu kuyasogeza mbele kutokana na ukosefu wa jukwaa la kuandalia mashindano yake.

Michezo ya Olimpiki inatarajiwa kuanza Julai 23 na kufikia tamati yake Agosti 9 ambapo Kenya inawakilishwa na mabondia 4.

Wakati huo, mwenyekiti wa ndondi Mombasa Abdulsalaam Kassim amesema mipango inaendelea kwa tawi la ndondi Mombasa kupata jukwaa la kuandalia mashindano yake.

Mombasa imekuwa bila jukwaa la kuandaliwa mashindano yake baada ya jukwaa la pekee lilipewa na kampuni ya mchezo wa kamari ya Sportpesa kupelekwa Nairobi kufanyiwa ukarabati.

“Nimekuwa na mazungumzo na viongozi kadhaa Pwani kuhusu kutununulia jukwaa na hivi karibuni tutakuwa na cha kujivunia,” akasema Abdulsalaam.

Mashindano kadhaa yameahirishwa Mombasa kutokana na swala la ukosefu wa jukwaa jambo ambalo mwenyekiti huyu ameahidi kulizika katika kaburi la sahau.

You can share this post!

Watu wa Rais waingia baridi

Chelsea kuvunja benki ili kumsajili Robert Lewandowski...