• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 12:38 PM
Chelsea kuvunja benki ili kumsajili Robert Lewandowski kutoka Bayern

Chelsea kuvunja benki ili kumsajili Robert Lewandowski kutoka Bayern

Na MASHIRIKA

CHELSEA wako radhi kuvunja benki na kumsajili fowadi matata wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Poland, Robert Lewandowski kwa kima cha Sh7.8 bilioni.

Hii ni baada ya juhudi za Chelsea kushawishi Borussia Dortmund kukubali ofa ya pesa pamoja na wachezaji kadhaa ili kufanikisha uhamisho wa chipukizi Erling Haaland ambaye bei yake ni Sh23.4 bilioni kuzaa nunge.

Hali hiyo imewaweka The Blues ambao ni mabingwa wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) kumhemea Lewandowski kadri wanavyopania kumtafutia kocha Thomas Tuchel fowadi wembe ambaye ni mwepesi wa kutikisa nyavu za wapinzani.

Hata hivyo, kibarua cha Chelsea cha kushawishi Lewandowski kutua uwanjani Stamford Bridge si chepesi ikizingatiwa kwamba matarajio ya Bayern ni kumpa sogora huyo mwenye umri wa miaka 32 mkataba mpya utakaomdumisha ugani Allianz Arena hadi 2023.

Lewandowski alivunja rekodi ya Gerd Muller mnamo 2020-21 baada ya kufunga jumla ya mabao 41 kwenye Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) muhula huo.

Kwa upande wake, Lewandowski amefichua hamu ya kunogesha soka katika ligi nyingine tofauti ya bara Ulaya kabla ya kuangika rasmi daluga zake ulingoni.

Kwa mujibu wa gazeti la Mirror Sport, Bayern hawatakuwa radhi kumtia Lewandowski mnadani kabla ya kupata sogora atakayejaza nafasi yake.

Chelsea wanajitosa katika vita vya kuwania huduma za Lewandowski siku chache baada ya Manchester City kujiondoa katika kinyang’anyiro hicho na kuelekeza mawazo yao kwa Harry Kane wa Tottenham Hostpur.

Tuchel anaamini kwamba ujio wa Lewandowski utapiga jeki kikosi cha Chelsea ambacho kimesalia bila fowadi mzoefu baada ya Olivier Giroud kuyoyomea Italia kuvalia jezi za AC Milan.

Chini ya Tuchel aliyeaminiwa kuwa mrithi wa Frank Lampard uwanjani Stamford Bridge mnamo Januari 2021, safu ya mbele ya Chelsea sasa inajivunia huduma za wavamizi Hakim Ziyech, Timo Werner, Christian Pulisic, Tammy Abraham na Callum Hudson-Odoi.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Mombasa yasitisha mashindano ya ndondi hadi michezo ya...

Chipukizi Oduor afungia Barnsley goli ikizima Sheffield...