• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 8:55 PM
Montreal yadumisha rekodi ya kutoshindwa MLS hadi mechi nne, imezima Inter Miami

Montreal yadumisha rekodi ya kutoshindwa MLS hadi mechi nne, imezima Inter Miami

Na GEOFFREY ANENE

CF Montreal anayochezea kiungo Mkenya Victor Wanyama imedumisha rekodi ya kutoshindwa hadi mechi nne kwenye Ligi uu ya Amerika na Canada (MLS) kwa kuzaba Inter Miami CF 1-0 mjini New Jersey, Jumapili.

Mathieu Choiniere alifungia Montreal bao hilo la pekee na la ushindi dakika ya 41 ugani Red Bull Arena.

Kiungo huyo mwenye umri wa miaka 22, ambaye alikuwa akishiriki mchuano wake wa kwanza wa MLS tangu Mei 15, alikamilisha pasi safi kutoka kwa kiungo Djordje Mihailovic kwa kumwaga kipa John McCarthy. Ni mara ya kwanza Montreal imemaliza michuano minne bila kupoteza tangu ilipofanya hivyo kati ya Juni 13 na Julai 7 mwaka 2018.

Nayo Miami, ambayo inanolewa na Muingereza Phil Neville na kujivunia kuwa na nyota wa zamani wa Real Madrid, Napoli, Juventus, AC Milan na Chelsea Gonzalo Higuain na Blaise Matuidi aliyechezea Paris Saint-Germain, imepoteza michuano mitano mfululizo.

Montreal ya kocha Wilfried Nancy ilidhibiti idara nyingi za mchezo huo zikiwemo umilikaji wa mpira kwa asilimia 52 dhidi ya 48, makombora yote 17-5 na shuti zilizolenga lango 7-3.

Wanyama, Aljaz Struna na Rudy Camacho walilishwa kadi ya njano kwa upande wa Montreal katika dakika 60 za kwanza. Nao, Leandro Pirez, Kelvin Leerdam na Magalhaes da Silva walionyesha kadi hiyo kwa upande wa Miami dakika 20 za mwisho. Montreal inashikilia nafasi ya nane kwa alama 16 kutokana na mechi 11.

Klabu hii inashiriki ligi ya MLS ya ukanda wa Mashariki. Viongozi New England Revolution wana alama 24 baada ya kujibwaga uwanjani mara 12.

You can share this post!

Renato Sanches sasa andazi moto linalowaniwa Arsenal na...

Corona hatari sana yaja hata kwa waliopata chanjo –...