• Nairobi
  • Last Updated May 2nd, 2024 2:19 PM
Morocco wapepeta Mali na kuhifadhi ubingwa wa taji la CHAN

Morocco wapepeta Mali na kuhifadhi ubingwa wa taji la CHAN

Na MASHIRIKA

MOROCCO ndiyo timu ya kwanza kutetea ufalme wa taji la CHAN baada ya kusajili ushindi wa 2-0 dhidi ya Mali jijini Yaounde, Cameroon mnamo Jumapili usiku.

Mabao yote mawili ya Morocco yalipachikwa wavuni kupitia mikwaju ya kona katika kipindi cha pili mbele ya mashabiki 6,700 waliokubaliwa kuhudhuria mchuano huo uwanjani Ahmadou Ahidjo.

Soufiane Bouftini alifungua ukurasa wa magoli katika dakika ya 69 kabla ya jingine kufumwa wavuni na Ayoub El Kaabi aliyejivunia jumla ya mabao tisa kwenye fainali za mwaka 2018 na kuongoza Morocco kutwaa kombe la CHAN mbele ya mashabiki wao wa nyumbani wakati huo.

Mali walikamilisha mchuano dhidi ya Morocco wakiwa na wachezaji 10 pekee uwanjani baada ya Issaka Samake kuondolewa uwanjani baada ya kuonyeshwa kadi mbili za manjano.

Awali, refa raia wa Kenya aliyekuwa mwamuzi kwenye fainali hiyo, alikuwa amewaonya Samake na Mohammed Ali Bemammer kwa maneno kabla ya wasaidizi wake kumshauri kurejelea tukio la Samake kupitia teknolojia ya VAR na hivyo kubatilisha maamuzi yake ya awali na kuchomoa kadi ya pili ya manjano.

Mali walianza mchuano huo kwa matao ya juu ikizingatiwa jinsi walivyotawaliwa na kiu ya kushambulia kwa nia ya kuendea mabao ya mapema ili kuvuruga mipango ya mabingwa watetezi.

Hata hivyo, ni Soufiane Rahimi wa Morocco ndiye aliyemtatiza pakubwa kipa na nahodha wa Mali, Djigui Diarra kabla ya Moussa Kone wa Mali kushuhudia kombora lake likidhibitiwa vilivyo na mlinda-lango wa Morocco, Anas Zniti.

Morocco walimiliki asilimia kubwa ya mpira katika kipindi cha pili na wakalalamikia kunyimwa mkwaju wa penalti iliyopuuzwa na refa katika dakika ya 55 baada ya kurejelewa kwa VAR.

Soufiane Rahimi alitawazwa mfungaji bora wa fainali za CHAN mwaka huu baada ya kufuma wavuni jumla ya mabao matano, yakiwemo mawili dhidi ya Cameroon kwenye hatua ya nusu-fainali.

Fainali hiyo ilihudhuriwa na Rais wa Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), Ahmad Ahmad na wanasoka wa zamani wa timu ya taifa ya Cameroon – Samuel Eto’o, Patrick Mboma na Jacques Songo’o.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Gor, AFC Leopards waumiza nyasi bure alasiri nzima

Shughuli zarejea kawaida baada ya shule iliyogeuza madarasa...