• Nairobi
  • Last Updated May 17th, 2024 8:50 AM
Mrembo mwenye azma ya kuvuna sifa kama Lionel Messi

Mrembo mwenye azma ya kuvuna sifa kama Lionel Messi

NA PATRICK KILAVUKA

LICHA ya wembemba wake na umri mdogo, mwanadada huyu ni moto wa kuotea mbali katika kusakata boli kama winga!

Aliwasha mshumaa wa talanta yake kama difenda. Ana matamanio ya kuwa mchezaji wa kitaifa na kimataifa kama Lionel Messi.

Pauline ‘Mamu’ Kakivi, 12, ni mwanafunzi wa Gredi ya Sita katika Shule ya Msingi ya St Martin’s, Kibagare, kaunti ndogo ya Westlands jijini Nairobi.

Yeye ni kitinda mimba katika familia ya watoto wawili wa Bw Nicholas Musee na Bi Lydia Mueni.

Alianza kudanadana kupiga soka akiwa na umri wa miaka tisa akiwa Gredi ya Tatu kabla talanta yake kutambuliwa na kocha Peter Nganga wa timu ya Kibagare Girls ambayo inashiriki ligi ya Kanda, FKF, Nairobi West na aliye mkufunzi wa soka anakosomea.

Kocha Peter anakiri kwamba, yeye ni mchezaji ambaye anachangamkia kandanda sana kwani mara ya kwanza alipohudhuria mazoezi, alipenda sana kufanya vimbunga vya soka na kudhihirisha kwamba ndani mwake, anayo talanta ambayo ilikuwa inaota ila, ilistahili kupigwa msasa.

Hapo ndipo alijitwika jukumu la kumnoga na mawaidha ya kuichongachonga.

Alianza kumwajibisha jukumu kama difenda.

“Kadri mazoezi yalivyozidi kupamba moto, alionyesha ana kasi ya kuchezeshwa winga, kuwa na chenga maridhawa, krosi na pasi za uhakika,” asema mkufunzi huyo na kuongezea kwamba anaona kama atafaa timu ya Harambee Starlets kutokana na jitihada zake kwenye mazoezi na vile anajitia moyo kufaulu licha ya changomoto za hapa na pale.

Isitoshe, ‘Mamu’ amejikuza sana kutokana na heshima yake kwa kila mchezaji na wadau wa timu, kuwa na nidhamu mchezoni na nje ya uwanja na kujipa moyo kutoboa katika soka.

Pauline Kakivi (wa pili kulia mbele) akiwa na kikosi cha Kibagare Girls ambacho kinashiriki ligi ya Kanda FKF, Nairobi West. PICHA | PATRICK KILAVUKA

Ukakamavu, ujasiri na nguvu za usuli huwaacha mashabiki na wachezaji vinywa wazi kutokana na chenga zake za maudhi na ufungaji wake magoli.

Katika shule ameshiriki katika soka kutokea kaunti ndogo ya Westlands hadi ya Kanda ya Nairobi ambapo alitia kimiani mojawapo ya magoli matatu ambayo walipiga kaunti ya Dagoretti. Isitoshe, aliisaidia timu yake mtaani kuibuka ya pili bora katika ngarambe ya Westlands Soccer Association.

Kwa sasa anafinyangwa kusakata katika timu kubwa katika ligi kwani kocha na wadau wana uhakika kwamba, atawajibishwa katika kikosi ambacho kitacheza msimu ujao kama njia ya kimuangazia na kumpa fursa ya kutanua kipaji chake.

Wachezaji ambao wanamvutia kutokana na upigaji soka ni mchezaji mwenza timuni straika Brenda Khatundis na Lionel Messi wa PSG ya Ligi Kuu ya Ufaransa

Timu ambazo anavutiwa kuzichezea ni Arsenal, Barcelona na Manchester City.

Pauline anaipongeza shule kwa kumpa fursa ya masomo licha ya kuwa na changamoto ya karo. Aidha, wadau wa timu mlezi Kibagare Girls kwa kukumbatia na kumtandikia zulia la kitalanta akilenga kutimiza ndoto yake ya kuwa mchezaji sugu wa kabumbu.

Pauline Kakivi akiwa na kocha Peter Nganga (kulia) na mzazi wake. PICHA | PATRICK KILAVUKA

Wakati wake wa ziada husaidia wazazi wake kufanya kazi za nyumbani kabla kuelekea uwanjani.

“Nimempa uhuru wa kukuza kipaji chake kwani niliona anapenda soka licha kwamba alikuwa anapenda kucheza netiboli lakini akahiari kujikuza kisoka,” anafichua mzazi wake.

Changamoto yake ni kupata vifaa vya mchezo kama sare, buti na kadhalika.

Hata hivyo, baada ya miaka mitano hivi amejiwekea malengo awe anaichezea timu ya taifa ya U-17 na U-20.

  • Tags

You can share this post!

Simba Queens yaingiza Afrika Mashariki nusu-fainali CAF

Man-United kuvaana na Barcelona katika mchujo wa kuingia...

T L