• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:09 PM
Msimu wa Supa Ligi (NSL) kuanza rasmi Novemba 26 kwa mechi tisa

Msimu wa Supa Ligi (NSL) kuanza rasmi Novemba 26 kwa mechi tisa

NA JOHN ASHIHUNDU

MSIMU mpya wa Supa Ligi (NSL) wa 2022/2023 utaanza rasmi Novemba 26 kwa mechi tisa katika viwanja mbali mbali, huku timu 29 zikishiriki.

Dandora Love na Muhoroni Youth zilizomaliza katika nafasi ya 19 na ya nne mtawalia zimebadilisha majina baada ya kupata wamiliki wapya, na sasa zitajulikana kama Kajiado FC na Darajani Cogo FC.

Baada ya kamati kuu ya FKF kupiga marufuku matokeo ya msimu wa 2021/2022 ulioendeshwa kwa kiasi fulani na Kamati ya Mpito, timu za APS Bomet na Fortune Sacco zilizokuwa zimefuzu kushiriki katika Ligi Kuu sasa zitabakia kwenye ligi hiyo ya NSL kujaribu bahati kwa mara nyingine.

Kwenye mechi za NSL zitakazochezwa Novemba 26, Darajani Cogo itaialika Mully Children Family (MCF) katika uwanja wa Hope Centre, wakati Naivas ikivaana na Mara Sugar ugani Camp Toyoyo.

Migori Youth ambao wamesajili wachezaji kadhaa kuongezea kikosi kigumu watakuwa nyumbani Awendo kukaribisha Murang’a Seal.

Kwenye mechi nyingine itakayochezewa Gusii Stadium, Kajiado FC watakuwa ugenini dhidi ya wenyeji, Shabana FC, huku Coastal Heroes ikipambana na majirani Mombasa Elite katika uwanja wa Mbaraki Sports Club.

Vihiga United wataanza msimu dhidi ya Fortune Sacco katika mechi itakayochezewa Wanguru Stadium, Mwea.

Ratiba ya mechi za Novemba 26 ni: Darajani Cogo v MCF (Hope Centre), Naivas v Mara Sugar (Camp Toyoyo), Migori Youth v Murang’a Seal (Migori Stadium), Fortune Sacco v Vihiga United (Wanguru Stadium, Mwea), Coastal Heroes v Mombasa Elite (Mbaraki Sports Club), Shabana v Kajiado FC (Gusii Stadium), APS Bomet v SS Assad (Bomet Stadium), Kibera Black Stars v Silibwet (Camp Toyoyo).

  • Tags

You can share this post!

Jezi za Ingwe zanunuliwa kama njugu

KOMBE LA DUNIA FIFA 2022: Timu zilizojipata makundini...

T L