• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 6:55 AM
Nabirye ateuliwa kikosi cha Uganda michuano ya AWCON

Nabirye ateuliwa kikosi cha Uganda michuano ya AWCON

NA RUTH AREGE

KIUNGO wa kati wa timu ya Ligi Kuu ya wanawake KWPL Vihiga Queens Joan Nabirye, ametajwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Uganda, Crested Cranes ambacho kinatarajiwa kucheza michuano ya Mataifa Bingwa Afrika (AWCON) Julai 2022 nchini Morocco.

Timu hiyo chini ya mkufunzi George William Latalo, ilipata tikiti ya kuwakilisha Afrika Mashariki baada ya timu ya taifa ya Kenya ya wanawake Harambee Starlets kujiondoa mashindanoni.

Nabirye anayesema ana umri wa miaka 22, alitwaa ubingwa wa nne wa Ligi Kuu akiwa na timu ya Vihiga Queens, ikiwa ni baada ya kumaliza msimu bila kupoteza mechi yoyote.

Vihiga Queens ilitoka sare tatu na kushinda mechi 20 kati ya mechi 23 ilizocheza.

Akizungumza na Taifa Spoti, alikiri kuwa, lengo lao kubwa msimu jana lilikuwa kuandikisha historia nyingine ya kutopoteza mechi yoyote ya ligi na kutwaa ubingwa.

“Msimu jana ulikuwa mgumu kwetu lakini tulipambana na kuandikisha rekodi nzuri. Tulitaka kuandikisha historia kwa kuwa sisi ni mabingwa na siku zote mabingwa lazima wajulikane kwa vitendo. Hilo lilidhihirika wazi,” alikiri Nabirye.

Aidha, alisema kuwa hana uhakika ikiwa ataendelea kusalia kwenye timu hiyo ya Vihiga msimu ujao.

Baada ya kufunga kazi nchini Kenya, alirejea nyumbani Uganda kwa mapumziko na baadaye aliitwa kujiunga na timu ya taifa ya Crested Cranes.

“Ni ndoto ya kila mchezaji kuchezea timu ya taifa lake. Habari hii niliipokea kwa furaha na nina imani nitawakilisha ukanda huu wa Afrika Mashariki vizuri. Najua mengi yanatarajiwa kutoka kwetu ila nina imani kuwa tutarejea nyumbani na taji,” aliongeza Nabirye.

Uganda ipo kwenye Kundi A pamoja na wenyeji Morocco, Burkina Faso na Senagal.

Timu ya Harambee Starlets haikuweza kushiriki kwenye michuano hii baada ya shirikisho la soka duniani FIFA, kupiga Kenya marufuku ya kutoshiriki michuano ya kimataifa.

Hata baada ya marufuku hayo, Kenya ilipanda ngazi kwenye jedwali la FIFA kutoka nafasi ya 147 hadi 146.

  • Tags

You can share this post!

Shirikisho kuandaa vipute vingi kunoa Wapwani katika magongo

Gor Mahia na Ingwe zavuna pakubwa kwa kupata mdhamini mpya

T L