• Nairobi
  • Last Updated May 1st, 2024 7:02 PM
Nation FC mabingwa wa Kombe la SJAK

Nation FC mabingwa wa Kombe la SJAK

NA TOTO AREGE

NATION FC inayomilikiwa na kampuni ya Nation Media Group (NMG), ndio mabingwa wa kombe la shindano la kandanda la Shirikisho la Waandishi wa Habari za Michezo nchini (SJAK) ambalo lilifanyika katika ukumbi wa Galleria Mall, Nairobi mnamo Jumamosi.

Nation FC ilishinda SuperSport 3-2 katika fainali.

Yasmin Khalid anayependwa na mashabiki, Eric Musungu na Titus Mbithi walifungia Nation bao kila mmoja, huku Janet Ongendo na Veran Mukanda wakifungia SuperSport.

Kwa ushindi huo, Nation FC ilijinyakulia kitita cha Sh50,000, SuperSport ikapata Sh30,000 huku CGTN wakirejea nyumbani na Sh20,000 kwa kumaliza katika nafasi ya tatu.

Nation FC ambao walikuwa wamepangwa katika kundi la kifo la “C” wamewazaba watani wao wa jadi Standard 5-1 katika mojawapo ya nusu fainali huku SuperSport wakiilaza CGTN 3-2 katika nusu fainali nyingine.

Nahodha wa Nation FC, Titus Mbithi amesema ilikuwa ni nyongeza ya ari kabla ya mechi dhidi ya NFT Autoports Freight katika Ligi ya Biashara siku ya Jumapili.

“Mchezo ulikuwa mgumu lakini nina furaha tumeshinda. Tunashukuru usimamizi wa Nation Media Group kwa usaidizi mkubwa na tunaweza kutarajia bora,” amesema Mbithi.

Katika mchujo wa kuwania nafasi ya tatu, CGTN walipata nafuu kutokana na kupoteza dhidi ya Super Sport na kuwalaza Standard 5-0.

Hafla hiyo iliyoambatana na Siku ya Kimataifa ya Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Duniani (AIPS) ilileta pamoja vyombo vya habari ikiwa ni pamoja na KBC, Royal Media Services, Radio Africa Group, Makueni FC, Athletic FC , Freelancer Journalists, MediaMax, KASS, Mozzart bet.

Mjumbe wa La Liga Alvaro Abreu amesema anatazamia uhusiano bora wa kufanya kazi na SJAK.

“Hii ni zaidi ya tulivyotarajia na kwa kweli nimefurahi kuwa shindano limetia fora. Tunatarajia kulifanya kuwa kubwa zaidi na bora zaidi. Tulidhani ni moja tu ya hafla nyingi ambazo tumeandaa lakini shindano likawa ni la ushindani ambao ulikuwa mzuri,” amesema Alvaro.

Mgeni mkuu, mwenyekiti wa zamani wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) Sam Nyamweya ametoa wito kwa wafadhili kuunga mkono malengo ya SJAK na matukio yajayo.

“Kwanza niwapongeze viongozi wapya wa SJAK na zaidi kwa kuandaa hafla hiyo ambayo imezikutanisha vyombo mbalimbali vya habari. Ili matukio haya zaidi yatokee, wanahitaji wafadhili wajitokeze kuunga mkono kazi zao. Nina furaha kuona vyombo vya habari vinapigania tuzo kuu,” amesema Nyamweya na kuongeza kuwa atahakikisha kwamba idhini ya mwanahabari kuripoti mechi za ligi inafanywa rahisi.

La Liga, KCB , DSTV na Safari Premium Drink walidhamini hafla hiyo.

  • Tags

You can share this post!

Wakazi wa Mombasa wakerwa na hatua ya EPRA kupandisha bei...

Nairobi City Marathon 2023  

T L