• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:05 PM
Nation FC yaanza mazoezi ya Betway Cup na msimu mpya, itapimana nguvu na Kabiru mnamo Jumatano

Nation FC yaanza mazoezi ya Betway Cup na msimu mpya, itapimana nguvu na Kabiru mnamo Jumatano

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya Nation FC imeanza mazoezi Jumanne baada ya miezi 12 kutokana na changamoto za janga la virusi vya corona ikijiandaa kwa Kombe la Rais wa Shirikisho la Soka Kenya (FKF) almaarufu Betway Cup.

Nation FC, ambayo inapata udhamini kutoka kwa kampuni ya Nation Media Group, itakuwa mgeni wa Vihiga Sportiff katika mechi ya raundi ya 64-bora uwanjani Mumboha Grounds mnamo Februari 13.

Mchuano huo utapisha ule kati ya Luanda Villa dhidi ya GDC uwanjani humo.

Akizungumzia maandalizi ya timu hiyo kutoka jijini Nairobi baada ya kipindi cha kwanza cha mazoezi, Kocha Mkuu John Ashihundu alikuwa mwingi wa furaha kurejelea mazoezi na pia kikosi kizima kujitokeza uwanjani katika Shule ya Upili ya St Mary’s mtaani Lavington.

“Wachezaji wote wamefika mazoezini. Mazoezi yamekuwa mazuri. Tatizo ni kuwa hatujakuwa mazoezini kwa muda mrefu,” alisema mwanahabari huyo na kufichua kuwa timu hiyo imejiongeza nguvu kwa kusaini kipa Stanslaus Atsango na kiungo mshambuliaji Bennis Otieno Onyango.

“Bennis ni mchezaji mzuri sana. Ataongeza makali yetu ya kutafuta mabao,” alisifu mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 21 ambaye ni mwanafunzi wa zamani wa Ramba Boys katika kaunti ya Siaya.

Kuhusu Atsango, Ashihundu alisema, “Tulitatizika msimu uliopita tulipokuwa na uhaba wa makipa. Nakumbuka kuna mechi moja tulipoteza kwa sababu tulikuwa na kipa mmoja katika hali nzuri na hakujitokeza uwanjani. Atsango atasaidiana na Georges Ipomai katika idara hiyo.”

Meneja wa timu hiyo Elias Makori pia alifurahia kurejea uwanjani baada ya muda mrefu. Alisema, “Mungu ni mzuri! Kuna kazi kubwa ya kupunguza uzani, lakini tunasubiri kwa hamu kubwa mchuano wa Betway Cup dhidi ya Vihiga Sportiff. Kushinda ama kupoteza si muhimu. Kurejea tu uwanjani ni ushindi kivyake!”

Makori alisema kutoka kikosi cha wachezaji 25 waliohudhuria mazoezi, 20 wataunda timu ya mwisho itakayoelekea Mumboha katika kaunti ya Vihiga mnamo Ijumaa asubuhi. Alifichua kuwa Nation itajipima nguvu dhidi ya wenyeji Kabiru kuamua jinsi kikosi cha kusafiri kitakavyopangwa.

“Mwaka uliopita tulibanduliwa na Jericho Revelation katika raundi ya kwanza kwa hivyo itakuwa hatua nzuri tukipita awamu hiyo msimu huu,” alisema.

Hii itakuwa mara ya nne Nation FC kushiriki kipute hiki ambacho mshindi atajikatia tiketi ya kuwakilisha Kenya katika Kombe la Mashirikisho la Afrika (Confederation Cup).

You can share this post!

Riise atema Mead na Nikita kwenye timu ya taifa ya soka ya...

Wito mchezo wa magongo upewe nafasi sawa na kandanda,...