• Nairobi
  • Last Updated May 19th, 2024 9:01 PM
Newcastle yabana Manchester United ligini

Newcastle yabana Manchester United ligini

Na MASHIRIKA

KOCHA Ralf Rangnick amekiri kwamba hakuridhishwa na matokeo ya kikosi chake kilicholazimishiwa sare ya 1-1 na Newcastle United katika mechi ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) mnamo Jumatatu usiku ugani St James’ Park.

Edinson Cavani alitokea benchi katika kipindi cha pili na kusawazishia Man-United waliojipata chini katika dakika ya saba baada ya Allan Saint-Maximin kuweka wenyeji Newcastle kifua mbele katika dakika ya saba.

Man-United walisuasua katika vipindi vyote viwili vya mchezo huku wakipoteza umiliki wa mpira kirahisi na kuzidiwa maarifa na Newcastle waliosalia imara katika safu zote.

Japo bao la Cavani lilihakikisha kwamba Man-United hawapotezi alama ya kwanza chini ya Rangnick ambaye ni kocha mshikilizi, alama moja dhidi ya Newcastle haikutosha kuwaweka Red Devils pazuri katika juhudi za kuwania nafasi ndani ya mduara wa nne-bora.

Kufikia sasa, Man-United ambao ni mabingwa mara 20 wa EPL wanashikilia nafasi ya saba kwa alama 28 sawa na nambari sita West Ham United. Ni pengo la alama saba ndilo linatenganisha Man-United na Arsenal wanaofunga orodha ya nne-bora.

Hata hivyo, masogora wa Rangnick wana mechi mbili zaidi za kutandaza ili kufikia idadi ya michuano ambayo imepigwa na Arsenal, nambari tatu Chelsea na mabingwa watetezi Manchester City wanaoselelea kileleni mwa jedwali kwa alama 47.

“Hatukudhibiti mchezo ila kwa dakika chache tu kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa kipindi cha kwanza kupulizwa. Vijana walikosa kiu ya kuwania mpira na wakatepetea katika kila idara,” akatanguliza Rangnick.

“Hofu ni kwamba washindani wetu wakuu wanazidi kutamba na pengo la alama kati yetu nao linazidi kupanuka. Matumaini ya nne-bora yanadidimia licha ya kwamba tuna mechi zaidi za kusakata,” akaeleza mkufunzi huyo raia wa Ujerumani.

Newcastle wangalifunga mabao zaidi katika kipindi cha pili ila juhudi za Miguel Almiron na Jacob Murphy zikzimwa na kipa David de Gea aliyefanya kazi ya ziada katikati ya michuma ya Man-United.

Alama moja iliyovunwa na Newcastle katika pambano hilo iliwadumisha katika nafasi ya 19 kwa alama 11 sawa na Burnley. Norwich City wanavuta mkia wa jedwali kwa alama 10. Pigo zaidi kwa Newcastle ya kocha Eddie Howe ni majeraha yaliyowaweka Saint-Maximin na Callum Wilson katika ulazima wa kuondolewa uwanjani katika kipindi cha pili.

Wakiwa miongoni mwa washiriki wa EPL ambao maandalizi yao kwa kipute hicho yalivurugwa na Covid-19, Man-United walishuka ugani kwa mara ya kwanza tangu Disemba 11 walipocharaza Norwich City 1-0 uwanjani Carrow Road.

Visa vya maambukizi mapya ya Covid-19 vilichangia kufungwa kwa kambi ya mazoezi ya Man-United na mechi zilizokuwa ziwakutanishe na Brentford kisha Brighton zikaahirishwa.

Man-United walitarajiwa kuendeleza ubabe uliowavunia ushindi wa 1-0 dhidi ya Crystal Palace na Norwich katika michuano ya awali ligini.

Tangu waagane rasmi na kocha Ole Gunnar Solskjaer aliyepigwa kalamu mnamo Novemba 21 ugani Old Trafford, Man-United sasa hawajashindwa katika mechi saba mfululizo kwenye mashindano yote. Isitoshe, wanajivunia rekodi ya kufunga bao katika kila mojawapo ya mechi ambazo wamepigia ugenini katika EPL kufikia sasa.

Kilichotarajiwa kutambisha Man-United ni rekodi nzuri ya kuchabanga Newcastle katika michuano minne ya awali huku wakifunga angalau mabao matatu katika kila mojawapo ya mechi hizo. Hata hivyo, Man-United sasa hawajawahi kukamilisha mechi bila kufungwa goli na Newcastle tangu Januari 2019.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

JUMA NAMLOLA: Serikali itumie maneno matamu kushawishi watu...

Mbappe na Lewandowski wapinga mpango wa FIFA kuandaa Kombe...

T L