• Nairobi
  • Last Updated May 8th, 2024 8:55 PM
Mbappe na Lewandowski wapinga mpango wa FIFA kuandaa Kombe la Dunia kila baada ya miaka miwili

Mbappe na Lewandowski wapinga mpango wa FIFA kuandaa Kombe la Dunia kila baada ya miaka miwili

Na MASHIRIKA

MSHAMBULIAJI Kylian Mbappe wa Paris Saint-Germain (PSG) na timu ya taifa ya Ufaransa na fowadi Robert Lewandowski wa Bayern Munich na timu ya taifa ya Poland, wamepinga mpango wa fainali za Kombe la Dunia kuandaliwa kila baada ya miaka miwili.

Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) limependekeza fainali za kipute hicho cha haiba kubwa kufanyika kila baada ya miaka miwili badala ya miaka minne kama sehemu ya kuimarisha zaidi kampeni za kivumbi hicho.

Kwa mujibu wa FIFA, kuandaliwa kwa fainali za Kombe la Dunia kila baada ya miaka miwili kutavuna kipato cha ziada cha pauni 3.3 bilioni juu ya kile ambacho kimekuwa kikipatikana kwa kawaida kipute hicho kinapoandaliwa kila baada ya miaka minne.

Shirikisho la Soka la bara Ulaya (Uefa), Ligi Kuu za bara Ulaya na Shirikisho la Soka la Amerika Kusini (Conmebol) ni miongoni mwa wadau waliopinga mpango wa Kombe la Dunia kuandaliwa kila baada ya miaka miwili.

Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) ni kati ya wadau ambao wameunga mkono pendekezo hilo.

FIFA imeshikilia kwamba fedha za kiingilio, haki za matangazo kupitia vyombo vya habari na udhamini iwapo kipute hicho kitafanyika baada ya miaka miwili zitaongezeka kutoka pauni 5.3 bilioni hadi pauni 8.6 bilioni kufikia 2030.

“Kombe la Dunia ni Kombe la Dunia. Ni kitu spesheli ndiposa kinafanyika kila baada ya miaka minne,” akatanguliza Mbappe aliyesaidia Ufaransa kutwaa Kombe la Dunia mnamo 2018 nchini Urusi.

“Ndicho kitu bora zaidi katika ulingo wa soka. Ndiyo mashindano bora zaidi duniani. Kukiandaa kila baada ya miaka miwili kutayeyusha ladha ya kipute hicho na kampeni zenyewe zitafanywa kuwa za kawaida mno kwa yeyote kushiriki. Hata si mashindano ya kawaida hata kidogo,” akaongeza.

“Tunacheza zaidi ya mechi 60 kwa mwaka. Kuna mapambano ya Euro, Kombe la Dunia na sasa UEFA Nations League. Tunafurahia kucheza lakini mashindano yakiwa mengi, tena hakuna raha ya kuyashiriki. Wachezaji pia huhitaji muda wa kupumzika na kujumuika na familia zao,” akasisitiza Mbappe katika kauli iliyoungwa mkono na Lewandowski.

“Iwapo watu wanataka kuona mchezo wa haiba kubwa na soka ya viwango vya juu inayotawaliwa na hisia kali za ushindani, basi ni vyema Kombe la Dunia lisalie kufanyika baada ya miaka minne. Ushindani na ubora wa viwango ndio hufanya Kombe la Dunia kuwa mashindano spesheli na tofauti kabisa na Euro au Nations League,” akasema Lewandowski.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Newcastle yabana Manchester United ligini

Washukiwa 10 wakamatwa kwa kuiba mali ya Sh3 milioni kutoka...

T L