• Nairobi
  • Last Updated May 12th, 2024 5:17 PM
Neymar sasa pua na mdomo kufikia rekodi ya Pele katika orodha ya wafungaji bora wa muda wote nchini Brazil

Neymar sasa pua na mdomo kufikia rekodi ya Pele katika orodha ya wafungaji bora wa muda wote nchini Brazil

Na MASHIRIKA

NYOTA Neymar Jr sasa amesalia na mabao tisa pekee kufikia rekodi ya kitaifa ya magoli 77 inayoshikiliwa na nguli wa soka Edson ‘Pele’ Arantes do Nascimento ambaye ni mfungaji bora wa muda wote kambini mwa Brazil.

Hii ni baada ya Neymar ambaye ni fowadi matata wa Paris Saint-Germain (PSG) kufunga bao lake la 68 ndani ya jezi za Brazil na kusaidia mabingwa hao mara tano wa Kombe la Dunia kuwaponda Peru 4-0 katika mchuano wa Kundi A kwenye fainali zinazoendelea za Copa America.

Brazil walijiweka uongozini katika dakika ya 12 kupitia bao la Alex Sandro wa Juventus. Neymar alipachika wavuni goli la pili la Brazil katika dakika ya 68 na kuikaribia rekodi ya Pele.

Mabao mengine ya Brazil yalifumwa wavuni kupitia kwa Everton Ribeiro na Richarlison na Andrade walioletwa uwanjani katika kipindi cha pili. Wenyeji Brazil sasa wanadhibiti kilele cha Kundi A kwenye Copa America ikizingatiwa kwamba waliwapepeta Venezuela 3-0 katika uwanja wa Nacional de Brasilia kwenye mchuano wa ufunguzi mnamo Juni 13, 2021.

Chini ya kocha Adenor ‘Tite’ Bacchi, Brazil kwa sasa wamefunga jumla ya mabao saba bila jibu kutokana na michuano miwili ya kwanza ya Copa America mwaka huu.

Brazil wanapigiwa upatu wa kutamalaki mechi zote za Kundi A na hatimaye kuhifadhi taji la Copa America. Watamenyana na Colombia katika mchuano wao wa tatu wa Kundi A mnamo Juni 24 kabla ya kufunga kampeni za makundi dhidi ya Ecuador mnamo Juni 28.

Neymar tayari amempiku fowadi wa zamani, Ronaldo Luis de Lima katika orodha ya wafungaji bora wa muda wote nchini Brazil.

Brazil ambao ni wafalme mara tisa wa Copa America, walitia kapuni ufalme wa kipute hicho kwa mara ya kwanza baada ya miaka 12 mnamo 2019. Makala ya 47 ya Copa America yanafanyika Brazil mwaka huu baada ya kuahirishwa mnamo 2020 kwa sababu ya janga la corona.

Vikosi vinne kutoka kwa kila kundi la timu tano ndivyo vitajikatia tiketi za kunogesha hatua ya robo-fainali.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Wakenya matumaini tele mashindano ya kutafuta tiketi ya...

Kituo cha afya cha Kiandutu sasa kutoa huduma bora za...