• Nairobi
  • Last Updated April 30th, 2024 2:58 PM
Kituo cha afya cha Kiandutu sasa kutoa huduma bora za maabara

Kituo cha afya cha Kiandutu sasa kutoa huduma bora za maabara

Na LAWRENCE ONGARO

WAKAZI wa Kiandutu wamepata afueni baada ya kupata maabara kwenye hospitali yao ya Kiandutu Health Centre mjini Thika.

Kwa muda mrefu, hospitali hiyo imekuwa na shida ya kufanya vipimo vya maradhi tofauti ambapo huduma hazikufikia viwango vinavyostahili.

Afisa mkuu wa Afya wa hospitali hiyo Dkt Patrick Munyua, alipongeza shirika la Rotary Club kwa ushirikiano na wakfu wa Jungle Foundation, kwa kufanya juhudi kuona ya kwamba maabara ya kuhudumia watu 400 kwa siku inaanza kufanya kazi.

Alieleza kuwa kwa muda mrefu wakazi wapatao 20,000 wa kijiji cha Kiandutu wamekuwa wakitegemea hospitali hiyo ambayo haingeweza kutekeleza matakwa yote ya matibabu kwa kukosa kufanya vipimo muhimu.

“Wakfu wa Jungle Foundation umekuwa katika mstari wa mbele kutetea kuwekwa kwa maabara hiyo katika kijiji hicho. Hatua hivyo itafanya wakazi hao sasa wapate afueni ya kupata matibabu ya haraka kwa kurejelea matokeo ya vipimo vyao,” alieleza afisa hiyo wa afya.

Wagonjwa wengi walikuwa wakitembea mwendo wa kilomita tatu kila siku kwenda kutafuta huduma katika hospitali ya Thika Level 5, kwa sababu ya kukosa huduma za haraka hospitalini Kiandutu.

Mnamo Ijumaa, kwa mara ya kwanza wagonjwa wengi walipata huduma ya haraka baada ya maabara hiyo kufunguliwa rasmi na shirika la Rotary Club kwa ushirikiano na wakfu wa Jungle Foundation.

Afisa huyo wa afya alipongeza vikundi hivyo viwili kwa kuonyesha ukarimu kwa kuwajali wakazi wengi wa Kiandutu.

“Hata wagonjwa wengi waliofika hapa wameonyesha nyuso za furaha wakisema wamefurahia mwelekeo uliochukuliwa wa kuwajali kama wagonjwa,” alisema afisa huyo wa afya.

Hospitali hiyo ya Kiandutu ilijengwa miaka 10 iliyopita lakini imekuwa na sehemu ndogo ya kufanya vimimo vya sampuli za wagonjwa.

Dkt Munyua alieleza kuwa baada ya kupata maabara mpya na nzuri, wauguzi watafanya kazi yao kwa haraka na wataweza kuhudumia wagonjwa wengi kwa wakati mmoja.

Wakazi wengi wa Kiandutu walifurika nje ya hospitali hiyo ili kushuhudia ufunguzi wa maabara hiyo mpya.

You can share this post!

Neymar sasa pua na mdomo kufikia rekodi ya Pele katika...

Sande Katumba analenga kuchezea AFC Leopards