• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 10:48 AM
Ni kisasi, vita vya ubabe kati ya Faith na Hassan fainali 1500m wanawake leo

Ni kisasi, vita vya ubabe kati ya Faith na Hassan fainali 1500m wanawake leo

Na MASHIRIKA

FAINALI ya leo ya mbio za 1500m wanawake kwenye Olimpiki za Tokyo nchini Japan, itakuwa jukwaa la vita vya ubabe kati ya Mkenya Faith Kipyegon ambaye ni bingwa wa Olimpiki na malkia wa dunia, Sifan Hassan wa Uholanzi.

Huku fainali hiyo ikiwa ya pili kati ya tatu ambazo Hassan atanogesha kwenye Olimpiki za mwaka huu, Kipyegon atapania kulipiza kisasi dhidi ya Mholanzi huyo aliyempiku Hellen Obiri na kuzoa dhahabu katika 5,000m mnamo Jumatatu.

Hassan ambaye pia ni bingwa wa dunia katika 10,000m, atashuka ulingoni hapo kesho kumenyana tena na Obiri kwenye fainali ya mbio hizo za mizunguko 12 na nusu.

Mbali na Hassan aliyesajili muda wa dakika 4:00.23 kwenye nusu-fainali za Jumatano, washindani wengine wakuu wa Kipyegon hii leo ni Freweyni Gebreezibeher wa Ethiopia na Muingereza Laura Muir aliyejiondoa kwenye mbio za 800m ili kumakinikia zaidi kivumbi cha 1500m.

Muda wa dakika 3:56.80 uliosajiliwa na Kipyegon kwenye mchujo wa Jumatano ndio wa nne bora zaidi kuwahi kuandikishwa katika nusu-fainali za 1500m wanawake kwenye historia ya Olimpiki.

Kipyegon alizoa dhahabu ya 1500m kwenye Olimpiki za 2016 jijini Rio de Janeiro, Brazil kwa dakika 4:08.92 mbele ya Genzebe Dibaba wa Ethiopia (4:10.27) na Mmarekani Jennifer Simpson (4:10.53). Hassan aliambulia nafasi ya tano wakati huo kwa dakika 4:11.23.

Kipyegon amesajili matokeo ya kuridhisha kwenye kampeni za Diamond League msimu huu ingawa alizidiwa maarifa na Hassan katika duru ya Florence, Italia mnamo Juni 10. Hata hivyo, alilipiza kisasi kwa kumpiku Hassan katika duru ya Monaco, Ufaransa mnamo Julai 4.

Hassan ambaye sasa ni mwiba mchungu kwa Wakenya, tayari amezoa dhahabu ya Olimpiki iliyotwaliwa na Vivian Cheruiyot katika 5000m mnamo 2016 jijini Rio na alimpokonya Kipyegon ubingwa wa dunia katika 1500m mnamo 2019 jijini Doha, Qatar.Kipyegon alinogesha Riadha za Dunia za 2019 mwaka mmoja baada ya kujifungua.

Licha ya kuwa mwakilishi wa pekee wa Kenya katika fainali ya leo, ameapa kuhifadhi ubingwa baada ya Winny Chebet na Ednah Jebitok kubanduliwa kwenye nusu-fainali za Jumatano.

“Muda niliosajili kwenye raundi za mchujo ni wa kuridhisha. Natarajia ushindani mkali kutoka kwa Hassan na Muir. Lakini niko tayari kwa kibarua kinachonisubiri,” akasema Kipyegon.

You can share this post!

Uganda yamruka Ruto kuhusu ziara yake iliyotibuka

Mmoja auawa kwenye mzozo kuhusu vijana wawili