• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:55 AM
Ni ndoto isiyowezekana kwa Liverpool kutwaa mataji manne msimu huu – Virgil van Dijk

Ni ndoto isiyowezekana kwa Liverpool kutwaa mataji manne msimu huu – Virgil van Dijk

Na MASHIRIKA

INGAWA Liverpool wanapigiwa upatu wa kujizolea mataji manne kwenye kampeni za msimu huu, beki na nahodha wa kikosi hicho, Virgil van Dijk, amesema “hiyo ni ndoto isiyowezekana”.

Liverpool walikomoa Chelsea kwa penalti 11-10 mwishoni mwa Februari 2022 na kunyanyua taji la Carabao Cup. Miamba hao wangali wanafukuzia ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Kombe la FA na ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Chini ya kocha Klopp, Liverpool kwa sasa wanakamata nafasi ya pili kwenye jedwali la EPL kwa alama 73, moja pekee nyuma ya viongozi na mabingwa watetezi Manchester City. Walidengua Benfica ya Ureno kwenye robo-fainali za UEFA na wakajikatia tiketi ya nusu-fainali dhidi ya Villarreal ya Uhispania. Sasa watamenyana na Chelsea kwenye fainali ya Kombe la FA baada ya kubandua Man-City kwenye nusu-fainali kwa mabao 3-2 ugani Wembley mnamo Aprili 16, 2022.

Watapepetana na Manchester United katika EPL mnamo Aprili 19 ugani Anfield kabla ya kuvaana na Everton na Tottenham Hotspur kwenye vibarua vingine vigumu vya EPL msimu huu.

Kuna uwezekano Liverpool wakutane na Man-City kwenye fainali ya UEFA msimu huu iwapo watadengua Villarreal nao Man-City wanaonolewa na kocha Pep Guardiola wabandue Real Madrid ya Uhispania kwenye nusu-fainali nyingine ya kipute hicho.

“Mjadala kuhusu uwezekano wa Liverpool kutwaa mataji manne unatuweka katika presha zaidi. Ni jambo lisilowezekana ndiposa hakuna kikosi kimewahi kujivunia ufanisi mkubwa kiasi hicho kutoka Uingereza. Ni ndoto ya kila mchezaji na kila timu kushinda kila pambano lakini yapo maazimio mengine ambayo ni vigumu kufikia,” akasema sogora huyo raia wa Uholanzi.

Van Dijk alirejea uwanjani kuwajibikia Liverpool mnamo Agosti 2021 baada ya jeraha baya la goti kumweka nje kwa miezi 10.

Liverpool walitandika Man-United 5-0 walipokutana katika mkondo wa kwanza wa EPL mnamo Oktoba 2021. Kocha mshikilizi wa Man-United, Ralf Rangnick amewahi kuwanoa wachezaji kadhaa wa Liverpool, akiwemo Naby Keita aliyekuwa kiungo wake kambini mwa RB Salzburg nchini Austria na RB Leipzig inayoshiriki Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga).

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Trailblazers, KPA zafinya wapinzani wao katika Voliboli

Ronaldo na mchumba wake Georgina waomboleza baada ya mtoto...

T L