• Nairobi
  • Last Updated May 11th, 2024 5:06 PM
Ni vigumu kubashiri EPL sasa!

Ni vigumu kubashiri EPL sasa!

Na MASHIRIKA

MKUFUNZI Pep Guardiola wa Manchester City amekiri kuwa ushindani mkali unaotamalaki kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu huenda ukashuhudia mshindi wa kipute hicho akianza kujidhihirisha katika raundi chache za mwisho wa muhula.

Hii ni baada ya Liverpool, Chelsea, Manchester United na Arsenal ambao pia ni wawaniaji halisi wa taji la EPL msimu huu, kushinda mechi zao za Jumamosi.

“Tutarajie ushindani mkali hadi wiki chache za mwisho. Kila kikosi kina azma ya kushinda ligi na washindani wote wameweka wazi malengo yao. Sitatarajii mabadiliko makubwa kwenye msimamo wa jedwali kabla ya mwaka huu kukamilika,” akatanguliza Guardiola.

Ushindi wa 1-0 uliosajiliwa na Man-City dhidi ya Wolves ugani Etihad ulidumisha mabingwa hao watetezi kileleni mwa jedwali la EPL kwa pointi 38.

Hata hivyo, ni pengo la alama moja pekee ndilo linatamalaki kati yao na Liverpool wanaojivunia pointi 37, moja zaidi kuliko Chelsea wanaofunga mduara wa tatu-bora.

Chini ya kocha Thomas Tuchel, Chelsea walipepeta Leeds United 3-2 uwanjani Stamford Bridge, Arsenal wakakomoa Southampton 3-0 uwanjani Emirates, Liverpool wakakung’uta Aston Villa 1-0 ugani Anfield, nao Man-United wakasajili ushindi sawa na huo dhidi ya Norwich City uwanjani Carrow Road.

“Sijui kitakachofanyika katika wiki na miezi michache ijayo. Bado ni mapema sana kubashiri mshindi wa taji la EPL muhula huu. Hata hivyo, maazimio yetu yako wazi – tunalenga ubingwa wa mashabiki wetu wana kila sababu ya kuthubutu kuota,” akasema Guardiola.

Mbali na Man-City, Liverpool na Chelsea ndio miamba waliopo pazuri zaidi kutawazwa wafalme wa EPL msimu huu ikizingatiwa ufufuo mkubwa wanaojivunia chini ya Tuchel na Jurgen Klopp mtawalia.

Chelsea ilikamilisha kampeni za ligi msimu jana katika nafasi ya nne kwa alama 19 nyuma ya Man-City.

Licha ya pengo dogo la alama linalotenganisha vikosi vitatu vya kwanza jedwalini, Tuchel amefichua kwamba matarajio makubwa kutoka kwa mashabiki yanatia masogora wake presha kubwa.

Kwa upande wake, Guardiola ameshikilia kwamba pamoja na ushindani mkali, mechi 16 ambazo zimesakatawa ligini kufikia sasa hazitoshi kuamua mshindi wa ligi.

Man-City kwa sasa wanajiandaa kumenyana na Leeds United ligini hapo kesho huku Wolves wakipepetana na Brighton siku moja baadaye.

Kwa upande wao, ushindi wa Man-United dhidi ya Norwich uliendeleza rekodi nzuri ya kutoshindwa kwa mabingwa hao mara 20 wa EPL chini ya kocha mshikilizi Ralf Rangnick.

Ilikuwa mara ya kwanza kwa Man-United kukamilisha mechi mbili mfululizo kwenye kampeni za EPL msimu huu bila kufungwa bao. Mara ya mwisho kwa rekodi hiyo kuwekwa na miamba hao ni kati ya Februari na Machi 2021 ambapo walisakata mechi nne bila kufungwa. Kwa sasa wameshinda mechi tatu mfululizo ligini kwa mara ya pili msimu huu.

Rangnick sasa ndiye kocha wa pili wa Man-United baada ya Ernest Mangnall mnamo 1903 kuwahi kuongoza kikosi hicho kutandaza mechi mbili za kwanza za EPL bila kufungwa bao.

  • Tags

You can share this post!

Tundo mfalme mpya mbio za magari nchini

Uhuru arejesha Jamhuri eneo ilikoanzia

T L