• Nairobi
  • Last Updated April 28th, 2024 9:50 AM
Uhuru arejesha Jamhuri eneo ilikoanzia

Uhuru arejesha Jamhuri eneo ilikoanzia

Na WANDERI KAMAU

RAIS Uhuru Kenyatta jana Jumapili alirejesha maadhimisho ya sherehe za Sikukuu ya Jamhuri katika Bustani ya Uhuru, Nairobi, ambako zilifanyika kwa mara ya kwanza Kenya ikianza kujitawala Desemba 12 1964.

Kwenye hotuba yake, Rais Kenyatta alisema hatua hiyo inalenga kuwafahamisha Wakenya kuhusu safari ambayo Kenya imepiga ili kufikia iliko.

“Hili linalenga kutukumbusha mchango uliotolewa na mababu zetu kutufikisha tuliko kama nchi. Ni kumbukumbu zinazopaswa kutukumbusha daima hatungefikia tuliko isingekuwa ni kujitolea kwao,” akasema Rais.

Sherehe hizo zilifanyika kwa mara ya kwanza katika bustani hiyo mnamo Desemba 12, 1964, baada ya Bw Kisoi Munyao kupandisha bendera ya Kenya katika Mlima Kenya na kutoa bendera ya ‘Union Jack’, iliyowakilisha utawala wa kikoloni.

Sherehe hizo ziliongozwa na hayati Mzee Jomo Kenyatta baba yake Rais Uhuru, ambaye alikuwa rais wa kwanza wa Kenya huru.

Hata hivyo, mtindo huo ulibadilika kadri miaka ilivyosonga, baada ya marais kama marehemu Daniel Moi, Mwai Kibaki na sasa Rais Kenyatta kuchagua viwanja vya michezo vya Moi (Kasarani) ama Nyayo kuadhimisha sherehe hizo.

Kinyume na ilivyokuwa awali, bustani hilo limefanyiwa ukarabati mkubwa chini ya usimamizi wa Jeshi la Kenya (KDF).

Serikali inasema muundo wake mpya unalenga kuwavutia Wakenya na wageni zaidi kuutembelea, kama mojawapo ya maeneo ya kihistoria nchini.

“Ni mojawapo ya njia za kulinda na kuhifadhi historia yetu,” akasema Katibu wa Usalama wa Ndani, Dkt Karanja Kibicho, ambaye ndiye aliongoza shughuli za maandalizi ya sherehe hizo.

You can share this post!

Ni vigumu kubashiri EPL sasa!

Kingi awaacha wafuasi wake kwenye mataa

T L