• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 7:55 AM
Nina imani na silaha mpya Shujaa – Simiyu

Nina imani na silaha mpya Shujaa – Simiyu

Na GEOFFREY ANENE

KOCHA Innocent Simiyu ana matarajio makubwa kutoka kwa wachezaji watatu wapya aliojumuisha Kenya Shujaa itakayowania ubingwa wa Raga za Dunia za wachezaji saba kila upande mjini Dubai.

Akizungumza baada ya kutaja wachezaji wapya Kevin Wekesa (Kabras Sugar) na Tony Omondi (Mwamba) na Edmund Anya (Impala Saracens) anayerejea kikosini tangu 2018-2019, Simiyu alisema aliridhishwa nao kwenye mashindano ya Safari Sevens jijini Nairobi mwezi Oktoba.

“Anya pia ana urefu mzuri utakaotusaidia katika mipira ya juu, Wekesa ana nguvu na tunamuona kama kizibo cha Andrew Amonde naye Omondi ana uongozi mzuri,” alieleza nahodha huyo wa zamani wa Shujaa.

Nelson Oyoo anarejea kama nahodha kuchukua nafasi ya Herman Humwa aliyefanya majukumu hayo wakati wa Safari Sevens ugani Nyayo. Oyoo amepona jereha la kinena alilopata katika duru ya pili na mwisho ya Raga za Dunia 2021 mjini Edmonton mnamo Oktoba 25.

Oluoch pia ametoka mkekani baada ya kupona kifundo naye Daniel Taabu aliyegongwa na kupoteza fahamu nchini Canada, yuko sawa kusaidia Shujaa katika azma yake ya kuwa na mwanzo mzuri msimu huu.

Shujaa, ambayo ilimaliza msimu 2021 katika nafasi ya tatu nyuma ya Afrika Kusini na Great Britain baada ya kuzoa alama 34, imesikitisha kwa miaka miwili mfululizo mjini Dubai kwa kupoteza mechi zake zote za makundi.

Itamenyana na Argentina, Amerika na Uhispania katika mechi za Kundi B mnamo Novemba 26. Duru ya kwanza itakamilika Novemba 27, huku ile ya pili ikiandaliwa Desemba 3-4 mjini humo. Shujaa itaelekea Dubai hapo Jumapili.

Kikosi Shujaa: Nelson Oyoo (nahodha), Herman Humwa, Alvin Otieno, Johnstone Olindi, Levi Amunga, Billy Odhiambo na Daniel Taabu.., Tony Omondi, Bush Mwale, Jeff Oluoch, Alvin Marube, Edmund Anya, Timothy Mmasi na Kelvin Wekesa.

Benchi ya kiufundi – Innocent Simiyu (Kocha Mkuu), Mike Shamiah (Naibu wa Kocha, ujuzi), Anthony Muchiri (Naibu wa Kocha, mazoezi ya nguvu na viungo), Lamech Francis (mnyooshaji wa misuli) na Erick Ogweno (Meneja).

You can share this post!

Mwatate FC yajipanga kupanda ngazi ligi kuu ya FKF licha ya...

Vuta nikuvute FKF kuvuruga soka nchini

T L