• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 5:55 AM
Vuta nikuvute FKF kuvuruga soka nchini

Vuta nikuvute FKF kuvuruga soka nchini

Na JOHN ASHIHUNDU

Baadhi ya makocha wazalendo wakiongozwa na Jacob Ghost Mulee, wamesema vuta nikuvute ya sasa kati ya Serikali na Nick Mwendwa itatumbukiza Kenya katika hatari ya kufungiwa kimataifa na kuuvuruga shughuli za mchezo huo nchini kwa jumla.

Lakini maoni yao yamepingwa na wenzao wengi wanaopendekeza heri Kenya ipigwe marufuku hadi watu wanaofaa wapewa mamlaka ya kusimamia mchezo ambao umedidimia tangu Mwendwa achukue usukani miaka sita iliyopita.

Makocha na wanasoka wa zamani wanaounga mkono Waziri Amina wamedai Mwendwa ameshindwa kuwajibikia pesa zilizotengewa uimarishaji wa soka nchini, ambapo maoni yao yameungwa mkono na timu nyingi za ligi kuu zikiongozwa na AFC Leopards na Gor Mahia.

Shirikisho la Kimataifa la Kandanda (Fifa) limetishia kuipiga Kenya marufuku baada ya Waziri wa Michezo, Utamaduni na Urithi- Amina Mohamed kuteua kamati ya muda kusimamia shughuli za kandanda kwa miezi sita.

Lakini Fifa imesisitiza kwamba Kenya itapigwa marufuku kushiriki katika mashindano yoyote ya kimataifa iwapo Serikali haitarejesha ofisini rais huyo wa Shirikisho la Kandanda Nchini (FKF) na kamati yake.

Shirikisho hilo la kimataifa linapinga serikali yeyote kuingilia masuala ya uendeshaji wa mashirikisho wanachama, lakini Kenya kupitia kwa Waziri wa Amina imepuuza onyo hilo na kusisitiza kwamba hatua ya kuondoa ofisi ya Mwendwa mamlakani itabakia vivyo hivyo.

Baada ya kuipiga marufuku FKF, Waziri Amina aliteua kamati ya muda chini ya Jaji Mstaafu Aaron Ringera kukaa kwenye usukani kwa miezi sita hadi uchaguzi huru ufanyike.Wakenya wanasubiri mawasiliano ya mwisho kutoka Fifa mara tu mkutano wa mwisho kati ya Amina na Katibu Mkuu wa Fifa, Fatma Samoura utakapomalizika mapema juma lijalo.

Mbali na kuathiri timu za taifa- Harambee Stars kwa muda utakaowekwa, kadhalika marufuku hii inamaanisha hakuna klabu yoyote ya soka nchini Kenya itakayokubaliwa kushiriki mashindano yoyote ya kimataifa.

Kwa mfano, iwapo hatua hiyo ingechukuliwa mapema Gor Mahia na Tusker hazingepangiwa kucheza na CS Sfaxien na Otoho d’Oyo katika mashindano ya CAF Confederation Cup mtawaliwa.Kadhalika timu ya akina dada inaweza kupoteza nafasi ya kucheza Uganda, Eritrea na Djibouti katika mechi za kuwania nafasi ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 (AWCON), huku wanasoka wetu wakikubaliwa tu kucheza katika ligi za nyumbani.

Marufuku hii kadhalika itawazuia wachezaji wetu kujiunga na klabu za ng’ambo, kwani Fifa haitatambua vyeti vyao vya ITC. Vile vile wachezaji wetu walio ng’ambo hawataruhusiwa kuhamia katika timu zingine.

Kadhalika waamuzi wazalendo hawatakuwabiliwa kuchezea mechi katika mataifa ya kigeni.Lakini Fifa imeonya kuwa Kenya imo hatarini kupigwa marufuku endapo haitatekeleza uamuzi wa Korti iliyoagiza Mwendwa afunguliwe mashtaka kwa muda usiozidi siku saba, la si hivyo akubaliwe kuendelea kuongoza FKF.

Kwenye barua ya Fifa iliyotumwa kwa Amina, Fifa ilisema uteuzi wa kamati ya Ringera unachukuliwa kama Serikali kuingilia kati kwa maswala ya kandanda, huku ikiongeza kwamba Fifa haikubali uendeshaji wa soka uingiliwe, kwani unaenda kinyume na kanuni zake ambazo haziruhusu uongozi wa kandanda uingiliwe.

Tunatarajia mazungmzo yanayoendelea kati ya Amina na Samoura, lakini Wakenya wengi wamesema heri kupigwa marufuku kuliko kumrejesha usukani Mwendwa.

You can share this post!

Nina imani na silaha mpya Shujaa – Simiyu

Wavamizi waua polisi, wateka Wachina 5 kambini

T L