• Nairobi
  • Last Updated May 18th, 2024 1:46 PM
Nottingham Forest warejea EPL baada ya miaka 23

Nottingham Forest warejea EPL baada ya miaka 23

Na MASHIRIKA

NOTTINGHAM Forest wataonja uhondo wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu ujao kwa mara ya kwanza tangu 1999 baada ya kukomoa Huddersfield Town 1-0 katika fainali ya mchujo wa kufuzu kwa kipute hicho kutoka Ligi ya Daraja ya Kwanza (Championship) mnamo Jumapili usiku ugani Wembley.

Ushindi huo mwembamba wa Forest walioanza msimu kwa kupoteza mechi sita kati ya saba, uliwavunia pia kima cha Sh25 bilioni utakaopiga jeki juhudi zao za kujisuka upya.

Walikamilisha kampeni zao za Champioship muhula huu katika nafasi ya nne kwa alama 80, mbili nyuma ya Huddersfield waliorejea kwenye EPL mnamo 2017 kabla ya kuteremshwa ngazi miaka miwili baadaye.

Forest sasa wanaungana na Bournemouth (alama 88) na mabingwa wa Championship, Fulham (90), kujaza mapengo ya Burnley, Watford na Norwich City walioshushwa daraja kwenye EPL mwishoni mwa muhula huu baada ya kujizolea pointi 35, 23 na 22 mtawalia.

Kibarua kikubwa zaidi kinachomkabili kocha Steve Cooper aliyejaza pengo la Chris Hughton kambini mwa Forest mnamo Septemba 2021, kujishughulisha vilivyo katika soko la uhamisho wa wachezaji wapya kadri anavyopania pia kumdumisha kiungo chipukizi, James Garner, 21, ambaye amekuwa akiwasakatia kwa mkopo kutoka Manchester United.

Forest ambao ni wafalme mara mbili wa European Cup, walijizolea alama moja pekee kutokana na mechi saba za ufunguzi wa muhula huu. Huo ulikuwa mwanzo mbaya zaidi kwao ligini chini ya kipindi cha miaka 108.

Hata hivyo, walijinyanyua upesi chini ya Copper aliyewahi kuongoza Swansea City kufuzu kwa fainali mbili za mchujo wa kufuzu kwa EPL. Walitinga ndani ya orodha ya sita-bora kwenye Championship kwa mara ya kwanza mnamo Februari 9.

Aidha, walizamisha Arsenal (1-0) na Leicester City (4-1) kwenye raundi za tatu na nne mtawalia za Kombe la FA kabla ya Liverpool walioishia kutawazwa wafalme kuwapepeta 1-0 katika robo-fainali mnamo Machi 20.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Wanne wazuiliwa siku saba kwa kutumia kileo kuwapumbaza...

Muthama apuuzilia mbali madai anataka kujiondoa UDA

T L