• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
Muthama apuuzilia mbali madai anataka kujiondoa UDA

Muthama apuuzilia mbali madai anataka kujiondoa UDA

NA CHARLES WASONGA

MWENYEKITI wa kitaifa wa chama cha United Democratic Alliance (UDA) Johnson Muthama amekana uvumi unaoenea mitandaoni kwamba anapanga kugura chama hicho na kujiunga na muungano wa Azimio la Umoja-One Kenya.

Kwenye taarifa kwa vyombo vya habari, Jumatatu, Mei 30, 2022, Seneta huyo wa zamani wa Machakos alikariri kuwa yu ndani ya muungano wa Kenya Kwanza na anaunga mkono azma ya urais ya kiongozi wa UDA William Ruto.

“Johnson Nduya Muthama haendi popote. Ningali mwenyekiti wa kitaifa wa UDA, chama kikubwa zaidi nchini. Huu ndio ukweli usiopingika. Nitasalia mwaminifu kwa UDA hadi tutakapounda serikali chini ya uongozi wa William Ruto,” Bw Muthama akasema.

Bw Muthama anayewania ugavana wa Machakos kwa tiketi ya UDA, aliisuta Azimio kwa kueneza uvumi huo na hivyo kusababisha hali ya taharuki ndani ya muungano wa Kenya Kwanza.

“Azimio la Umoja-One Kenya ni mateka wa uwongo unaovuja katikati ya ukweli. Wasidhani kuwa sisi kama UDA tunaweza kuamini uwongo na jumbe feki wanazoeneza kupitia mitandao ya kijamii,” akaongeza.

Uvumi huo ulienea saa kadhaa baada ya Naibu Mwenyekiti wa UDA Kipruto Arap Kirwa alitangaza kugura chama hicho na kujiunga na Azimio.

Bw Kirwa, ambaye zamani alihudumu kama Mbunge wa Cherangany na Waziri wa Kilimo, alitoa tangazo hilo katika mkutano wa Azimio uliofanyika katika eneo bunge la Sirisia, kaunti ya Bungoma, Jumapili, Mei 29, 2022.

Alipokelewa rasmi na mgombea urais wa muungano huo Raila Odinga pamoja na mgombea mwenza wake Martha Karua.

Kirwa alisema alichukua hatua hiyo baada ya kukerwa na kile alichokitaja kama kuteuliwa kwa mgombea mwenza wa Dkt Ruto, Rigathi Gachagua, kwa njia iliyokiuka misingi ya kidemokrasia.

Mbunge wa Kathiani Richard Mbui Jumatatu asubuhi alidai kuwa huenda Bw Muthama pia angegura kutoka kwa UDA kwa kile alichotaja kama kushindwa kwake kushiriki jukwaa moja na Gavana wa Machakos Dkt Alfred Mutua.

“Kwa sababu William Ruto amemkumbatia Dkt Mutua ambaye alijiunga juzi na Kenya Kwanza, sioni kama Seneta wangu wa zamani ataendelea kusalia katika muungano wa Kenya Kwanza,” akasema Bw Mbui katika kipindi cha mahojiano katika runinga ya Citizen.

Tangu Dkt Mutua alipotangaza kujiunga na Kenya Kwanza mapema mwezi wa Mei, Bw Muthama amekwepa kuhudhuria mikutano miwili katika kaunti ya Machakos.

Mnamo mwezi wa Februari 2022 aliyekuwa Mwekahazina wa UDA Omingo Magara, alilalamikia ukosefu wa demokrasia ndani ya chama hicho.

  • Tags

You can share this post!

Nottingham Forest warejea EPL baada ya miaka 23

TUSIJE TUKASAHAU: Mradi wa Arror umekwama licha ya ripoti...

T L