• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 11:55 AM
NYOTA WA WIKI: Callum Wilson

NYOTA WA WIKI: Callum Wilson

NA GEOFFREY ANENE

CALLUM Wilson ni mmoja wa wachezaji wanaong’ara kambini mwa Newcastle United, maarufu Magpies, katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Katika michuano saba ambayo Newcastle walisakata mwezi jana, straika huyo alichana nyavu za Manchester United na Tottenham (mara moja kila moja) na West Ham, Everton na Southampton (mara mbili kila moja).

Raia huyo wa Uingereza ana jumla ya mabao 15 pamoja na pasi nne zilizotumbukizwa wavuni ligini msimu huu.
Aliibuka mchezaji bora wa Newcastle wa Aprili.

Pointi 18 walizozoa – kati ya 21 zilizokuwa mezani – mwezi huo zimeshuhudia kikosi hicho kikijiweka pazuri kurejea katika kabumbu ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) tangu msimu 2003-2004.

Wilson, ambaye amekuwa akiwania nafasi moja na Alexander Isak na kutumiwa zaidi kutoka benchi (mara tisa katika mechi 17), ni mzuri wa kukimbia na mpira ili kusogeza timu yake karibu na maeneo hatari ya wapinzani.

Yuko sawa pia kupokea mipira ndani ya kijisanduku cha upinzani, kuwania mipira ya juu na kufuma mabao safi.

Wilson alilelewa kisoka na akademia ya Coventry City. Iliwahi kumpeleka kwa mkopo katika klabu za Kettering na Tamworth.

Alipata msukumo wa kujituma katika klabu hizo ndogo akitumai kuwa sogora wa kulipwa ili kujitafutia riziki na pia kuipa familia yake maisha mazuri.

Wilson alichezea Coventry jumla ya mechi 55 akiifungia mabao 23 na kumega asisti saba zilizoishia nyavuni, kabla kujiunga na Bournemouth mwaka 2014 kwa kima cha Sh557.3 milioni.

Alikuwa mali ya Bournemouth uwanjani Vitality hadi aliponyakuliwa na Newcastle mnamo Septemba 2020 kwa bei ya Sh3.3 bilioni.

Baadhi ya mataji ya kibinafsi ambayo amepata ni pamoja na kuwa mchezaji bora wa mwaka wa Coventry msimu 2013-2014 na wa Newcastle 2020-2021.

Kimataifa, Wilson amechezea timu ya watu wazima ya Uingereza mara sita tangu Novemba 2015 na kuifungia goli moja.

Mashindano ya haiba ambayo ameshiriki kikosini Three Lions ni Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar, alikomegea Jack Grealish pasi iliyozalisha goli Uingereza ikilipua Iran 6-2 mechi ya Kundi B.

  • Tags

You can share this post!

TAHARIRI: Mchango wa Ingwe ni muhimu katika soka

Mfalme Charles III atawazwa rasmi kwenye sherehe babukubwa

T L