• Nairobi
  • Last Updated May 4th, 2024 3:24 PM
NYOTA WA WIKI: Ciro Immobile

NYOTA WA WIKI: Ciro Immobile

NA GEOFFREY ANENE

CIRO Immobile anaongoza katika kutesa makipa kwenye Ligi Kuu ya Italia (Serie A) msimu huu.

Mchezaji huyo, ambaye ni mshambulizi, amecheka na nyavu mara 27 katika michuano 30 ligini humo. Amefikisha magoli 32 katika mashindano yote msimu huu. Atapata fursa ya kuimarisha idadi hiyo dhidi ya Sampdoria leo Jumamosi usiku.

King Ciro anavyofahamika kwa jina la utani, amepitia zaidi ya klabu 10 kabla ya kutulia kambini mwa Lazio ambako anafanya makubwa hayo.

Safari yake ya soka ilianzia katika klabu yake ya mtaani ya Torre Annunziata mwaka 1996.

Alinyakuliwa na na timu ya makinda ya Juventus kwa Sh9.8 milioni mwezi Agosti 2007. Hakuridhisha kambini mwa Juventus iliyompeleka Siena, Grosseto na Pescara kwa mkopo kati ya Julai 2010 na Juni 2012 kabla ya kumpiga mnada kwa Genoa kwa Sh490 milioni.

Alirejea Juve tena kwa Sh337 milioni kabla ya kuelekea Torino kwa Sh1.6 bilioni. Hapa, King Ciro aling’ara msimu 2013-2014 akiibuka mfungaji bora wa Serie A kwa magoli 22 katika michuano 33.

Alinyakuliwa na miamba Borussia Dortmund, ambao wamejipatia sifa ya kupalilia vyema talanta za makinda, kwa Sh2.2 bilioni mwaka 2014. Hata hivyo, Ligi Kuu ya Ujerumani ilimkataa na akayoyomea Sevilla nchini Uhispania kwa mkopo kwa msimu 2015-2016. Alinunuliwa na Sevilla kwa Sh1.3 bilioni Januari 2016, akitua Torino kwa mkopo kabla ya kupata makao Lazio mnamo Julai 2016 kwa Sh1.1 bilioni.

Tangu ajiunge na Lazio amekuwa ameaminiwa kwa ufungaji wa mabao. Amejaza nyavuni jumla ya magoli 182 katika michuano 258 amechezea Lazio pamoja na kusuka pasi 46 zilizoishia kuwa mabao. Anafukuzia taji lake la tatu la mfungaji bora wa Serie A kambini mwa Lazio baada ya kuona lango mara 29 msimu 2017-2018 na mara 36 msimu 2019-2020.

Kimataifa, Ciro amewakilisha Italia katika michuano 55 na kupachika mabao 15. Alikuwa mmoja wa wachezaji waliokosolewa vikali sana wakati Italia ililemewa na North Macedonia 1-0 katika mechi ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia 2022.

Sifa

Ciro Immobile ndiye mfungaji wa magoli mengi ya Lazio katika mashindano yote (189). Pia, anashikilia rekodi ya ufungaji wa mabao ya Lazio kwenye Serie A (150). Aliyeshikilia rekodi hizo ni Silvio Piola aliyechezea Lazio kwa misimu tisa kati ya 1934 na 1943. Immobile ni mwanasoka wa nne tu kufunga mabao zaidi ya 25 ligini katika ligi tano kubwa barani Ulaya kwa angaa mara tatu tangu msimu 2016-2017 baada ya Robert Lewandowski, Lionel Messi na Cristiano Ronaldo. Aliandikisha rekodi hiyo Aprili 24 alipofungia Lazio ikipoteza 2-1 dhidi ya AC Milan.

Kuzaliwa: Februari 20, 1990, Torre Annuziata, Italia

Jina: Ciro Immobile

Wazazi: Baba (Antonio Immobile), Mama (Michaela Immobile)

Ajenti: Alessandro Moggi

Nahodha: Ciro Immobile

Mkufunzi: Maurizio Sarri

Waajiri wakati huu: Lazio

Mmiliki mkuu: Claudio Lotito

Uwanja: Stadio Olimpico

Ligi: Serie A (Italia)

Waajiri wa zamani: Torre Annuziata, Salernitana & Maria Rosa Salerno, Sorrento, Juventus, Siena, Grosseto, Pescara, Torino (Italia), Dortmund (Ujerumani), Sevilla (Uhispania)

Ujira: Sh17.6 milioni kila wiki

  • Tags

You can share this post!

Liverpool vs Spurs patachimbika leo!

Brentford yazamisha chombo cha Southampton katika EPL

T L